Thursday, June 22, 2017

KATIBU MKUU UTUMISHI ASISITIZA NIDHAMU KWA VIONGOZI NA WATUMISHI NCHINI.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi na watumishi wote nchini kuzingatia nidhamu kama msingi wao wa utendaji kazi pamoja na kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili utumishi wao uweze kuwa mzuri.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo alipokutana na watumishi Mkoani Singida na kusikiliza matatizo, kero, changamoto pamoja na kupata maoni ya namna ya kuboresha utumishi wa umma kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma nchini.

Amesema kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu ya hali huku akiwasisitiza viongozi hasa wa watumishi wa umma kuwasikiliza watumishi wao pale wanapotoa maoni yao bila kuyapuuzia au kuwakatisha tamaa kwa vitisho.

“Ukiwa kiongozi unapaswa uweze kuishi na kila aina ya mtu, kuna watumishi wengine hawawezi kufichaficha mambo ukikosea wanakusema bila kupepesa maneno, wengine ni waoga hawawezi kukueleza wazi ila wanatumia mbinu mbali mbali, ukiwa kama kiongozi uwe tayari kupokea ushauri ili uweze kuboresha utendaji wako”, amesisitiza Dkt Ndumbaro.

Dkt Ndumbaro amewaasa viongozi hao kuwapongeza watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu ili iwe motisha kwa wale wavivu huku akiwataka kuwachukulia hatua wale wazembe na ambao hawataki kufuata kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

“Unakuta mtumishi anajituma anafanya kazi kwa bidii, ana nidhamu na ni mbunifu lakini wewe kiongozi wake unamuangalia tu bila hata ya kumpongeza, hiyo inakatisha tamaa, inatakiwa umpongeze sio lazima umpe fedha hata barua tu ya kutambua utendaji wake itampa hamasa yeye na wenzake. Lakini pia kuna mwingine anakuwa hatekelezi wajibu wake unamtazama tu, hapo utawakatisha tamaa hata wale wachapakazi, amesema.

Aidha amewapongeza watumishi wenye vyeti halali huku akieleza kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi bado ni endelevu ili kuhakikisha watumishi wanaobaki serikalini ni wale wanaostahili tu huku akiwashauri watumishi kuhakikisha wanasafisha taarifa zao muhimu ziwe halali na sahihi.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi amemshukuru Katibu Mkuu Utumishi kwa kuwatembelea watumishi wa Mkoa wa Singida na kusikiliza changamoto pamoja na maoni yao huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa bidi na nidhamu.

Dkt Lutambi amesema watumishi Mkoani Singida wanaadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya kazi kwa bidi pamoja na kuongeza muda wa kufanya kazi kutoka saa tisa na nusu mchana mpaka saa kumi na nusu jioni ili kutoa muda zaidi wa kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Linno Mwageni amemshukuru Katibu Mkuu Utumishi kuutembelea Mkoa wa Singida na kutoa maoni yake kuwa ili kuboresha utendaji hasa wa serikali za Mitaa inabidi serikali iwaajiri watendaji wa vijiji na kata wa kutosha.

Mwageni amesema watekelezaji wa shughuli na miradi ya serikali kwa ngazi ya mwananchi hasa ni watendaji wa vijiji na kata ambao kwa sasa ni wachache hivyo serikali iwaajiri wa kutosha ili waweze kufuatili kwa ukaribu miradi hiyo.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma.
 Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro alipowatembelea katika kuadhimisha wiki ya utumishi umma.
 Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida Mwalimu Eva Mosha akitoa maoni yake kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro aliwapotembelea watumishi wa Mkoa wa Singida katika kuadhimisha wiki ya Utumshi wa Umma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi na Kushoto kwake ni Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Nsajigwa.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Linno Mwageni akimshukuru Katibu Mkuu Utumishi kuutembelea Mkoa wa Singida pamoja na kutoa maoni yake ya kuboresha utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akiandika maoni na changamoto za watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi.

No comments: