Wednesday, June 14, 2017

Hatimae 'Pedeshee Ndama' huru kwa dhamana.

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

Baada ya kufanikiwa kulipa faini ya milioni 200 hatimae leo mfanyabiashara , Ndama Shabani Hussein, maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng'ombe amepata dhamana.

Ndama amepata dhamana baada ya kuwa na wadhamink wawili na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 600.

Wiki iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimtia hatiani Ndama na kumuhukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya milioni 200 baada ya kukiri shtaka la kutakatisha USD 540,000.

Aidha mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ilimsomea masharti ya dhamana mshtakiwa huyo iwapo angefanikiwa kulipa kiasi hicho cha milioni 200 ili awe huru katika mashtaka matano yanayoendelea kumkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.

Katika masharti hayo, Ndama alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu kiasi cha USD 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya milioni 600 mahakamani hapo ama mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha

Licha ya kupata dhamana, Ndama amerudishwa gerezani kukamilisha taratibu kabla ya kuachiwa huru. 

Hukumu hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na kuyakubali maelezo ya awali na maelezo yote yanayounda shtaka hilo la kutakatisha fedha, akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo yanayounda shtaka hilo, hawana kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha.

Pia mahakama ibebe dhana ya sheria hiyo ambayo lengo lake ni kuzuia makosa ambayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa kosa ambalo mshtakiwa amelifanya.

Kwa upande wa Wakili Wabeya Kung’e anayemtetea mshtakiwa huyo kwa kushirikiana na Jeremiah Mtobesya, Kung’e aliiambia mahakama kuwa ni wazi mshtakiwa amekiri kosa baadaya kusomewa maelezo ya awali ni rai yetu mahakama isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa .

Aliiomba mahakama izingatie maombi yao kwa sababu mshtakiwa huyo hilo ndiyo kosa lake la kwanza, kitendo chake cha kukiri kosa kinaonesha kusikitikia kosa alilolitenda na kwamba anayo familia ambayo inamtegemea ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa ndani imepata shida kwa kukosa huduma yake.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 13(a) cha sheria ya kutakatisha fedha ni rai yetu mahakama tukufu isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu amejutia kosa alilolitenda”Alisisitiza kueleza Kung’e. Hivyo amehukumiwa kulipa faini ya Sh 200 milioni ama akishindwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Juni 6,2017 Ndama aliiomba mahakama akumbushwe shtaka, akakumbushwa na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na akalikubali shtaka hilo.

Akisomewa maelezo ya awali mahakamani hapo, Ndama alikubali maelezo ya awali aliyosomewa ikiwamo nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika kuingizwa hizo fedha, hundi 18 zilizotumika kutolea hizo fedha, maelezo ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.

Amekubali kuwa Mei 14,2013 wakurugenzi ambao pia ni wanahisa wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited wanaotambulika Brela, Bushoboka Mutamura na Mujibu Hamis Taratibu waliisajili kampuni hiyo Brela na kupata hati ya usajili namba 99249 kwa ajili ya kushughulikia biashara ya madini.

Aliendelea kukubali kuwa Septemba 16,2013 alifungua akaunti benki ya Stanbic katika tawi la Viwandani kwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwamo TIN namba ya kampuni hiyo, leseni ya biashara na hati yake ya kusafiria nakwamba wakati akiifungua alijitambulisha kuwa yeye ndiyo Mwenyekiti wa kampuni hiyo na mtia saini pekee.

Pia alikubali kuwa kampuni ya kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliingia mkataba na kampuni ya Trade TJL DTYL Limited ya Australia na kwamba aliwagaia wabia wenzake fedha hizo taslimu kwa lengo la kuficha chanzo chake.

Katika shtaka hilo la sita la kutakatisha fedha Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Ndama alilikubali shtaka hilo na kukana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Miongoni mwa mashtaka yanayoendelea kumkabili, Ndama anadaiwa Februari 20, 2014 Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboxi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Aidha anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

Shtaka lingine anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionesha kampuni ya Muru imeyawekea bima maboxi manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.

Anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya atawapa na kusafirisha dhahabu hizo. Kesi hiyo itatajwa Juni 16,2017.

No comments: