Monday, June 5, 2017

DKT NCHIMBI ATOA RAI KWA VYUO KUTOA WASOMI WENYE TIJA NA SIO KUTENGENEZA MIGOMO.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (katikati) akipiga ngoma kwa furaha kama ishara ya kuzindua kikundi cha Bright Focus kilichopo chuo cha Uhasibu Singida, kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo.
1
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia wanakikundi cha Bright Focus (hawapo pichani) kikundi hicho kipo chuo cha Uhasibu Singida.
2
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (katikati) akipiga ngoma kama ishara ya kuzindua kikundi cha Bright Focus kilichopo chuo cha Uhasibu Singida, kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo.
3
Wanachuo ambao ni wanakikundi cha Bright Focus kilichopo Chuo cha Uhasibu Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati wa uzinduzi wa kikundi hicho.
4
Makamu wa rais wa Bright Focus John Gama akiwasilisha malengo ya kikundi hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati wa uzinduzi katika chuo cha Uhasibu Singida.
………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa rai kwa vyuo vikuu na vyuo vinavyotoa elimu ya juu kuwa sehemu ya kuwafundisha na kuwatengeneza wasomi wenye kutambua fursa na tija za maisha na sio sehemu ya kuendekeza migomo isiyo na faida katika maisha ya wanachuo hao.

Dkt. Nchimbi ametoa rai hiyo jana wakati akizindua kikundi cha Bright Focus kilichopo chuo cha Uhasibu tawi la Singida chenye wana kikundi 89 ambao ni wanachuo, walimu na walezi wenye malengo ya kutambua fursa za kuboresha maisha.

Amesema wakati akizindua kikundi hicho anatambua kuwa kikundi hicho kitasaidia kubuni mawazo yenye tija, fursa, na mwelekeo wa kuboresha uchumi huku akiwasisitiza kuelekezana namna bora ya matumizi ya rasilimali walizonazo hususani rasilimali fedha.

Dkt Nchimbi amekitaka kikundi hicho kuwa chachu ya mabadiliko ya tabia na mienendo yote mibaya iwe mizuri kutokana na baadhi ya wanachuo katika vyuo mbalimbali kuhusishwa na tabia zisizo njema.

Amesema kila mwanakikundi anapaswa anatakiwa mawazo yake yaendane na malengo ya kikundi cha Bright Focus kuanzia mwenendo wa maisha yake, ufaulu wake na hata matumizi ya rasilimali yawe yenye muono wa kutengeneza faida na hasa kujifunza namna ya kuhifadhi akiba.

Aidha Dkt Nchimbi amekubali ombi ya wana kikundi hao la kuwa mlezi wao huku akiwaasa kutoegemea kwenye changamoto bali wazitazame fursa zilizopo huku akiwapongeza kwa kuanzisha kikundi hicho.

Akiwasilisha malengo ya kikundi hicho Makamu wa rais wa Bright Focus John Gama amesema kikundi kina malengo mengi ikiwemo kutoa udhamini kwa wanachuo ambao watashindwa kulipa ada kutokana na sababu mbalimbali.

Gama ameongeza kuwa kikundi kitaanzisha miradi ya maendeleo kama vile kilimo, biashara ya bajaji na pikipiki, ufugaji wa nyuki na kuanzisha makapuni mbalimbali ziku za baadaye ili wana kikundi waweze kujiongezea kipato.

Amesema kikundi kina lengo la kutatua changamoto ya ukosefu wa uzoefu hasa linapokuja suala la ajira kwa kuwaajiri wana chuo katika makampuni watakayoanzisha ili waweze kupata ujuzi huo pamoja na kuandaa ziara za mafunzo.

Katika uzinduzi wa kikundi cha Bright Focus kulikuwa na mdahalo wa nani ana umuhimu zaidi kati ya mwanamke na mwanaume ambapo wana kikundi walichangia hoja, kila upande wa mwanamke na mwanaume ukijitahidi kuthibitisha yale wanayoamini.

Dkt Nchimbi alihitimisha mdahalo huo kwa kusisitiza kuwa thamani ya mwanamke na mwanaume iko sawa kwakuwa katika jamii hakuna maendeleo yanayoletwa na mwanaume peke yake au mwanamke peke yakena hivyo kuwataka wazitambue thamani walizonazo na kuzienzi.

No comments: