Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) Tawi la Tanzania imekabidhi kisima cha maji, ndoo na vikombe vya kuchotea maji kwa Shule za Msingi Nyamagana A na B za Jiji la Mwanza.
Hafla ya kukabidhi kisima hicho pamoja na ndoo 24 na vikombe vilivyogharimu zaidi ya shilingi milioni 4.5, ilifanyika mwanzoni mwa juma hili ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Meya wa Jiji la Mwanza ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamagana (CCM) Bw. Bhiku Kotecha.
Akizungumza kabla ya kukabidhi kisima hicho, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania Bw. Sibtain Meghjee alisema kisima hicho kitazisaidia shule hizo na kuepuka gharama kubwa za malipo ya ankara za maji na aliuomba uongozi wa shule hizo uhakikishe unakitunza kisima hicho vizuri ili kidumu.
Alisema kuwa baadaye taasisi hiyo itaangalia jinsi ya kubadili mfumo unaoweza kutunzika kikamilifu kwa kuweka tanki la kuhifadhia maji na mota ya kusukuma maji kutoka kisimani hadi kwenye tenki hilo ili maji yafike maeneo yote kwa urahisi.
Akizungumza kwa niaba ya walimu na wanafunzi wa shule hizo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamagana B Bw. Anatory Mnono alisema msaada huo umekuja muda muafaka kwani utawapunguzia mzigo mkubwa uliokuwa umewaelemea.
“Msaada huu wa kisima umetupunguzia changamoto ya malipo ya maji na kweli mzigo huu ulituelemea mno.Tutayatumia maji haya kuboresha mazingira ya shule zetu kwa kupanda miti, kufanya usafi na matumizi mengine ya kawaida.Tunaishukuru sana Taasisi ya The Desk & Chair, ” alisema.
Bw. Mnono alieleza kuwa si mara ya kwanza kwa taasisi hiyo kuzisaidia shule hizo za Nyamagana A na B zenye jumla ya wanafunzi 772 na walimu 27 kwani pia iliwahi kuwajengea matundu 24 ya vyoo kwa matumizi ya walimu na wanafunzi pamoja na kuwapa madawati zaidi ya 200 na kukarabati vyumba vya madarasa na madawati yote mabovu.
Naibu Meya wa Jiji la Mwanza ambaye pia ni Diwania wa Kata ya Nyamagana (CCM) Bw. Bhiku Kotecha akizindua kisima cha maji kilichokabidhiwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania kwa Shule za Msingi za Nyamagana A na B mwanzoni mwa juma hili ambapo diwani huyo alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kukabidhi msaada huo.Kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw. Sibtain Meghjee.
Naibu Meya wa Jiji la Mwanza ambaye pia ni Diwania wa Kata ya Nyamagana (CCM) Bw. Bhiku Kotecha akizungumza wakati akizindua kisima cha maji kilichokabidhiwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania kwa Shule za Msingi za Nyamagana A na B mwanzoni mwa juma hili ambapo diwani huyo alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kukabidhi msaada huo.Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw. Sibtain Meghjee.
Kotecha akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wanafunzi wa shule za Nyamagana A na B
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyamagana Anatory mnono akizungusha mkono wa kisima cha maji kulia ni Mwenyekiti wa The Desk & Chair Sibtain Meghjee, na kushoto ni Naibu Meya wa jiji la Mwanza Bhiku Kotecha
No comments:
Post a Comment