Thursday, June 1, 2017

Balozi Seif azindua Ofisi ya Taasisi ya Msaada wa Kisheria Visiwani Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  amewaomba Wananchi wote Visiwani Zanzibar kuzitumia huduma zinazotolewa na Wasaidizi wa Kisheria ili kuongeza ulinzi wa Haki za binaadamu, upatikanaji  wa haki na kuchangia katika kujenga jamii inayoishi kwa upendo na amani.
Alisema Wananchi wenye kipato duni ambao ndio wahanga wa ukiukwaji wa sheria na haki wanaweza kupata suluhu na ufumbuzi wa matatizo yao ya kisheria yanayowakabili watapoamua kutumia huduma hizo.
Akizindua Rasmi  uwepo wa Ofisi ya Taasisi ya Msaada wa Kisheria  Visiwani Zanzibar {LSF} usiku huu hapo  Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini  Balozi Seif Ali Iddi alisema hatua hiyo ni muhimu katika upatikanaji wa Haki na usimamizi wa huduma za msaada wa Kisheria katika Jamii.
Balozi Seif  alisema bado zipo changamoto nyingi zilizothibitisha wazi kwa Jamii kutoelewa vilivyo uwepo wa wasaidizi hao wa Kisheria licha ya kwamba huduma wanazotowa  hazihitaji malipo yoyote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitanabahisha Jamii kwamba Taasisi ya Msaada wa Kisheria {LSF} inaendelea kusaidia Taasisi zinazojihusisha na ulinzi wa Haki za Bianaadamu kupitia Fedha wanazozipata kutoka Mashirika ya Kimataifa ya Misaada ya DANIDA  na UKAID wakiweka mkazo zaidi kuwasaidia Wanawake.
 “ Wasaidizi wa Taasisi hii ni muhimu sana kwa vile wanatoka katika sehemu ya wanajamii wenyewe, wakiaminika, kukubalika pamoja na kutambua changamoto za jamii husika wakishiriki vyema katika utatuzi kwa kushirikiana na wahusika wa pande zote ”. Alisema Balozi Seif.
Alisema Serikali inapenda kuona  watu wengi wanakuwa na uelewa wa masuala ya Sheria na Haki zao ambapo Wanawake wanaweza kupata  haki zao hasa katika umiliki wa rasilmali ardhi, elimu pamoja na fursa za  kiuchumi zilizokuwa zikitawaliwa na mfumo Dume.
Balozi Seif alizishauri Taasisi zote zinazopata ruzuku ya fedha kutoa Taasisi hiyo ya Msaada wa Kisheria { LSF} kufanya kazi kwa bidii na ueledi ili kufanikisha malengo yaliyowekwa kupitia mpango maalum wa Taasisi hiyo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahitaji kutambua  matokeo ya msaada  unaotolewa katika kuhudumia Jamii ambao utawafanya watu wengi hususan wanawake na wananchi wenye kipato duni wanafanikiwa kupata huduma za msaada wa Kisheria.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishukuru Taasisi ya Msaada wa Kisheria     { LSF } kwa kutambua umuhimu wa kuwepo kwa huduma za Msaada wa Kisheria na Elimu ya Kisheria kwa watu wengi wa Zanzibar.
Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi wa Taasisi hiyo ya Kisheria kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaangalia  namna nzuri ya kufanya mapitio na kuongeza  wigo wa sheria  zilizopo ikiwemo sheria ya utoaji wa Huduma za Kisheria ili kuziimarisha zaidi.
Alielezea matumaini yake kuwa Vyombo vya Habari Nchini vitakuwa msaada mkubwa katika kuielimisha Jamii juu ya uwepo wa huduma muhimu za Msaada wa Kisheria Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuzitumia vyema.
Mapema Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria Bwana Kees alisema Wasaidizi wa Kisheria wapatao 4,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanaendelea kutoa msaada wa Kisheria kwa Wananchi Maskini katika kufikia suluhu ya matatizo yao.
Bwana Kees alisema huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ni  bila ya malipo na wasaidi wake  wanajitolea kufanya kazi kubwa inayopaswa kuigwa na kupongezwa katika kuwasaidia wana Jamii kupata haki zao.
Afisa Mtendaji huyo wa LSF ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi inayosimamia Sekta ya Sheria Zanzibar kwa juhudi zilizochukuliwa na kufikia hatua ya kufunguliwa Ofisi ya Taasisi hiyo Visiwani Zanzibar.
Naye kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa Omar Othman Makungu alisema Sheria ya msaada wa Kisheria imeshapitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kutiwa saini na Rais John Pombe Magufuli kufanya kazi Tanzania Bara ikiwatambua Wasaidizi wa Kisheria  kuwa ni watoa huduma za Kisheria.
Jaji Omar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia  Wizara inayosima Katiba na Sheria Zanzibar inafanya mipango katika kuhakikisha sheria kama hiyo inapelekwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupata baraka ya kuanza kufanya kazi Visiwani Zanzibar. 

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/6/2017.

No comments: