Brass band ya Chipikizi ikiongoza maandamano ya wakunga na wauguzi kupita mbele ya mgeni rasmi Waziri Afya Mhmoud Thabit Kombo katika maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mama Mariyam Othmani Mihale akiongoza wakunga na wauguzi katika wimbo maalum wa maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani katika ukumbi wa Wasanii Rahaleo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wuguzi na Wakunga Zanzibar Amina Abdulkadir Ali akitoa maelezo juu ya siku ya Wuguzi duniani katika maadhimisho yaliyofanyika ukumbi wa wasanii Rahaleo.
Mwakilishi wa Shirika linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) Zanzibar Sabina Luoga akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo katika Ukumbi wa wasanii Rahaleo Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na wakunga na wauguzi walioshiriki maadhimisho ya siku ya wakunga duniani yaliyofanyika ukumbi wa wasanii Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi Waziri wa Afya Zanzibar na viongozi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga na Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika Rahaleo Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Hospitali na Vituo vya Afya vya Wilaya vinaweza kupunguza idadi ya akinamama kujifungulia Hospitali kuu ya Mnazimmoja iwapo juhudi za kuandaa mazingira mazuri zitachukuliwa na wakunga na wauguzi wa vituo hivyo.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo.
Amesema akinamama wengi wamejenga imani ya kujifungua Hospitali kuu ya Mnazimmoja na kupelekea upungufu wa nafasi katika Hospitali hiyo huku vituo vya Afya vijijini vikiwa na akina mama wacheche wanaokwenda kwa huduma ya kuzaa.
Ameongeza kuwa Hospitali ya Mnazimmoja inazalisha zaidi ya akinamama 50 kwa siku na Mwembeladu wanawake 30 wengi wao kutoka vijijini wakati vituo vya afya vya huko vinazallisha wanawake wawili hadi watano kwa siku.
Waziri Mahmoud amewataka wakunga na wauguzi wa vituo vya afya vya Wilaya vinavyotoa huduma ya kuzalisha kuandaa mazingira yatakayowavutia wanawake kujifungua katika vituo vyao.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na mkakati wa kuandaa mazingira mazuri na kuweka miundo mbinu bora ikiwemo vifaa vya kisasa hivyo amewataka wafanyakazi nao kubadilika na kuwapa faraja wagonjwa ili wajenge imani kwao.
Amesema Serikali imetoa kibali cha kuajiri wafanyakazi wa sekta ya afya 201 kuanzia fani ya ukunga mpaka madaktari bingwa ili kuondosha upungufu wa wafanyakazi wa kada hizo katika Hospitali na vituo vya afya.
Amewataka wakunga na wauguzi kujenga moyo wa upendo, huruma na kuweka mbele maadili ya kazi na kuwahudumia wagonjwa bila ya kuwabagua kwa rangi, kabila ama nyadhifa zao na kutumia lugha nzuri.
Aidha amewashauri kutumia fursa walizonazo kujiendeleza kitaaluma kwa vile nafasi zipo katika vyuo vya ndani na nje ya nchi na Wizara iko tayari kuwasaidia.
Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Zanzibar (ZNMC) Amina Abdulkadir Ali amesema lengo kubwa la siku ya wauguzi Duniani ni kutoa mwamko kwa wananchi juu ya mchango wa wakunga katika jamii na kuwa pamoja nao.
Katika risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wakunga Zanzibar (ZANA) Valeria Rashid Haroub wameeleza changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa vitendea kazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua na uhaba wa madaktari bingwa katika kiliniki hizo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ‘Wakunga, Akinama na Familia ni washirika wa kudumu’. Ukiwa na maana ya kufanyakazi kwa karibu na familia, sio mama peke yake katika kutunza familia pamoja na kuwalinda watoto katika afya bora na kuwaepusha katika vitendo vya ukatili.
No comments:
Post a Comment