Wednesday, May 31, 2017

WATATU WALIOSHITAKIWA KWA KESI YA MADAWA YA KULEVYA WAACHIWA HURU


Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia kesi washtakiwa watatu waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya milioni 25 na kuamuru wasikamatwe.

Amesema washtakiwa hao wasikamatwe na kushtakiwa kwa kufunguliwa shtaka linalofanana na hilo labda kwa maelekezo ya Mahakama Kuu.

Hatua hiyo ua kufuta kesi hiyo imekuja baada ya washtakiwa kuwa rumande kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya upelelezi kukamilika na jalada ya polisi kutokuwepo mahakamani mara kadhaa. Washtakiwa walioachiwa huru ni, Salma Juma , Amos Sosoma na Rashid Mtitu.

Kesi hiyo iliyokuwa na namba 21 ya mwaka jana imefutwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage baada ya kukaa mahakamani hapo kwa miaka mine bila ya upelelezi kukamilika.

Amesema Machi 6, mwaka huu, mahakama iliamuru upande wa mashtaka ifikapo Machi 23, itoe taarifa juu ya hatua ya upelelezi lakini ilipofika siku hiyo upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na jalada la polisi halipo.

Akiendelea kusoma uamuzi huo Hakimu Mwijage alisema kesi iiahirishwa hadi Aprili 5, mwaka huu lakini upande wa mashtaka ulibaki na jibu lile lile kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe nyingine.

Hata hivyo baada ya kauli hizo kuebndelea kutawala mahakamani hapo mara kadhaa, washtakiwa walilalamika kuwa walifikishwa mahakamani Agosti 26, 2013.Walidai kuwa, kesi yao ilipita katika mahakama mbalimbali mbapo Juni 14, 2016 waliachiwa huru lakini walikamatwa tena na kupandishwa mahakamani hapo na kuendelea kusota rumande.

Katika kesi hiyo ambayo waliachiwa huru kabla ya kukamatwa tena walikuwa wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi kilo 920, zenye thamani ya milioni 138.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mwijage amesema upande wa mashtaka Juni 14, 2016 uliwafungulia kesi nyingine mbele yake wakidaiwa kukutwa na gramu 169,500 za dawa za kulevya aina ya Bangi zenye thamani ya Sh 25, 425,000.

Hakimu Mwijage alisema tangu Juni 14, mwaka jana hadi Aprili 5,mwaka huu, upelelezi haujakamilika na wala Upande wa mashtaka hawana jalada la [polisi.

“Tunawezaje kupiga vita dawa za kulevya kama upelelezi hauwezi kukamilika kwa zaidi ya miaka mitatu, magerezani kuna mrundikano wa mahabusu na kuna kesi za Meno ya Tembo na dawa za kulevya ambazo upelelezi wake unacheleweshwa bila ya kuwepo sababu za msingi.”Amesema Mwijage.

Ameongeza mahakama ipo kwa ajili ya kutenda lakini wanachokifanya upande wa mashtaka siyo kuendesha kesi bali ni kuwanyanyasa washtakiwa.“Kwa maoni yangu kesi ya jinai siyo ya kuchezea, shauri hili lilipaswa kusikilizwa Mahakama Kuu kutokana na hoja na malalamiko ya washtakiwa, mahakama hii inayo mamlaka ya kuchukua hatua na kutoa maamuzi.” Amesema Hakimu Mwijage.

Alibainisha kuwa anafahamu kwa mujibu wa sheria hakuna muda wa upelelezi wa kesi kama ya aina hiyo, ila amezingatia mazingira ya kesi , malalamiko ya washtakiwa, na taarifa upelelezi haujakamilika kwa siku 1335.

Amesema kitendo cha kucheleweshwa kukamilika kwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo imeonesha hakuna ushahidi dhidi ya washtakiwa kwa nia ya kutenda haki na kuepuka kwenda kinyume na sheria mahakama imeifuta kesi hiyo na kuamuru washtakiwa hao wasikamatwe na kushtakiwa kwa kufunguliwa shtaka linalofanana na hilo labda kwa maelekezo ya Mahakama Kuu.

No comments: