Sunday, May 21, 2017

WANAWAKE 18 WAHITIMU MAFUNZO YA UONGEZAJI THAMANI MADINI



Na Veronica Simba - Arusha

Jumla ya wanawake 18 kutoka mikoa mbalimbali nchini, jana (Mei 19, 2017) wamehitimu mafunzo ya ukataji na ung'arishaji madini ya vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kilichopo jijini Arusha. 

Wahitimu hao wa awamu ya nne, wamefanya idadi ya waliohitimu tangu kuanzishwa mafunzo husika katika Kituo hicho kufikia 65.

Akizungumza katika sherehe za Mahafali hayo, Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, alitoa wito kwa wadau wa madini ya vito nchini, kuwapa ajira na ushauri wa kitaalam wahitimu, ili waweze kujiajiri katika shughuli za uongezaji thamani madini. 

"Lengo ni kuhakikisha kuwa ukataji unafanyika kwa viwango vya kimataifa ili kuweza kuuza zetu kwenye masoko ya nje."

Aidha, Dkt. Pallangyo alitoa changamoto kwa wadau wote wa madini ya vito kuendelea kukuza shughuli za uongezaji thamani madini kwa kubadilishana uzoefu na wakataji wa madini ya vito mahiri duniani. 

"Kwa wale wafanyabiashara wa madini ya vito, mlioajiri wataalam wa kigen, natoa rai muendelee kuwahimiza watoe mafunzo kwa watanzania wanaofanya nao kazi, ili kuhawilisha utaalam huu adimu," alisisitiza. 

Vilevile, Naibu Katibu Mkuu, aliwaasa wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa Kituo kinachotoa mafunzo hayo ya TGC, kwa kuendelea kufanya shughuli za uongezaji thamani madini popote watakapokwenda. 

Alitoa rai kwa uongozi wa TGC kujenga utamaduni wa kuwaalika wahitimu wote wa Kituo hicho hususan waliojiajiri, kushiriki katika sherehe za Mahafali, ili waoneshe bidhaa zao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, akitoa historia ya TGC, alisema kuwa, Wizara ya Nishati na Madini iliamua kuwekeza katika Kituo hicho kwa malengo ya kutoa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa madini hayo. 

Aliongeza kuwa, malengo mengine ni pamoja na kukuza na kufanikisha shughuli za uongezaji thamani katika madini ya vito nchini, kukuza na kuendeleza ujuzi na ufahamu wa kutambua madini ya vito na kuongeza kipato na ajira kwa watanzania. 

Alisema kuwa, katika kujenga uwezo wa ndani na kupata wakufunzi wenye sifa za kimataifa; Wizara ilipeleka watumishi watatu nje ya nchi kujifunza masomo ya vito na usonara kwa lengo la kuwa wakufunzi katika Kituo hicho. "Watumishi hao walikwishahitimu mafunzo yao na tayari wamesharipoti kituoni."

Mhandisi Mchwampaka alisema kuwa, Wizara inakusudia kupeleka watumishi wengine watano nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo husika ili kukijengea uwezo Kituo kwa kuwa na walimu wa kutosha. 

Akizungumzia mafunzo mengine yanayotarajiwa kutolewa na Kituo hicho baadaye, alisema kuwa ni pamoja na Jemolojia, Utengenezaji wa bidhaa za mapambo pamoja na uchongaji wa vinyago vya mawe. 

"Aidha, Kituo kitaanzisha maabara ya utambuzi na uthibitishaji wa madini ya vito na bidhaa za urembo. 

Akisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi, kwa niaba ya wahitimu wenzake, Theresia Mollel, alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa uwezo kama wanawake wa kufanya kazi katika sekta ambayo wengi hudhani wanawake hawaiwezi. 

"Kupitia mafunzo haya, tunaihakikishia jamii kuwa wanawake tunaweza kufanya mabadiliko katika tasnia ya madini ya vito na kuleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla."

Kituo cha Tanzania Gemological Centre (TGC) kilianzishwa mwaka 2003.

Mafunzo haya hutolewa kwa muda wa miezi saba ambapo miezi sita ni nadharia (darasani) na mwezi mmoja ni mafunzo kwa vitendo.

Wanafunzi hawa wanafadhiliwa na Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Kamati ya Maonesho ya Madini ya Vito ya Arusha (Arusha Gem Fair) chini ya Mfuko wa Kuwaendeleza Wanawake.

 Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mwenye koti la mauamaua), akikagua kazi za uongezaji thamani madini ya vito, zinazofanywa katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kilichopo jijini Arusha.

 Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mwenye koti la mauamaua), akikagua kazi za uongezaji thamani madini ya vito, zinazofanywa katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kilichopo jijini Arusha.



Wahitimu wa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), wakiwa darasani.



Wahitimu wa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), wakiwa darasani.



Wahitimu wa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), wakiwa darasani.

 Wahitimu wa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), wakiwa darasani.

 Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mwenye koti la mauamaua), akijumuika pamoja na wahitimu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kucheza muziki.

 Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, akisoma historia ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kwa Mgeni Rasmi (hayupo pichani).



Mgeni Rasmi katika sherehe za mahafali ya Nne ya Mafunzo ya uongezaji thamani madini ya vito nchini, Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mwenye koti la mauamaua – walioketi) na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kulia kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu.



Mwanafunzi bora, Happiness Ernest, akipokea zawadi yake kutoka kwa Mgeni rasmi.

No comments: