Tuesday, May 16, 2017

Wananchi wa Pemba wahimizwa kuchangamkia fursa za EAC


Wananchi wa Pemba wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi katika Soko la EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewataka wakazi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia ipasavyo fursa za Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kujiongezea kipato. 

Mhe. Waziri alieleza kuwa katika ulimwengu wa leo hakuna nchi duniani itakayoweza kujiimarisha kiuchumi peke yake bila kushirikiana na nchi nyingine. Ndio maana hata zile nchi zilizoendekea kama Marekani na nchi za Ulaya wana umoja wao kwa madhumuni ya kuongeza nguvu na kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

Waziri Mahiga aliyasema hayo alipokuwa anafungua semina kuhusu elimu ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake kwa wananchi wa Pemba ambayo itatolewa na wataalamu wa Wizara yake kwa siku nne kuanzia leo kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Gombani.

Mhe. Waziri alieleza kuwa kabla, wakati na baada ya ukoloni nchi za Afrika Mashariki zilikuwa na aina moja au nyingine ya Ushirikiano kwa madhumuni ya kuimarisha uchumi wa nchi zao, waliotutawala. Aina moja ya Ushirikiano ni ule Umoja wa Huduma ambao ulianzishwa mwaka 1961. Umoja huo ulianzisha mashirika mbalimbali kama vile bandari, ndege, hali ya hewa, posta na reli ambayo yalikuwa yanaendeshwa kwa pamoja.

Alisema Tanzania ipo katika eneo la kimkakati ndani ya Jumuiya ikiwa ni pamoja na kuwa na eneo kubwa kuliko nchi zote, idadi kubwa ya watu, ukanda mkubwa wa bahari na ardhi nzuri yenye rutuba na kihistoria Pemba ni eneo lenye rutuba nzuri kuliko maeneo yote ya Afrika Mashariki. Hivyo, kutokana na sifa hizo hakuna budi wananchi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla kujipanga vizuri ili kuchangamkia fursa hizo badala ya kubaki kuwa watazamaji na walalamikaji.

Waziri Mahiga aliongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina sifa nyingine ya pekee ya kuwa Muungano wa nchi mbili na kutoa wito kwa washiriki wa semina hiyo kutumia sifa ya umoja wao kuziendea na kuzichangamkia fursa za kiuchumi zilizopo kwenye Mtangamano.

"Nchi nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla zilijaribu kuungana lakini zilishindwa, kwa mfano nchi za Ghana, Mali na Guinea, nchi za Afrika zinazozungumza kifaransa, nchi za Misri na Syria, nchi za Afrika ya Kati na nchi za Pembe ya Afrika". “Ni sisi peke yetu hadi leo tumedumisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo juzi tu tuliadhimisha miaka 53 ya muungano huo”. Waziri Mahiga alisema. 

Aliendelea kuueleza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kudumisha Muungano huo ambapo kwa maneno yake alisema kuwa unaonewa wivu Afrika na duniani kote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Khamisi Juma Mwalim aliwasihi washiriki wa semina hiyo kuzingatia mafunzo yanayotolewa katika semina hiyo ili waweze kunufaika katika shughuli zao ikiwemo ujasiriamali.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dar es Salaam, 15 Mei, 2017
Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kisiwani Pemba. Semina hiyo inatolewa kwa wajasiriamali wa Pemba ili waweze kuchangamkia fursa za mtangamano. Semina hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Uwanja wa mpira wa Gombani. 
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria semina hiyo, wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Konde Mhe. Mbarouk Ali akiwa pamoja na washiriki wengine wakifuatilia kwa makini ufunguzi huo 
Sehemu nyingine ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga hayupo pichani. 
Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Zanzibar Mhe. Khamis Juma Maalim akisoma hotuba ya ukaribisho. 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi naye akielezea jambo kwenye ufunguzi wa semina hiyo ya Mtangamano wa Afrika Mashariki. 
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Sanday markert kutoka Pemba, Bw.Khamis Suleiman Masoud akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hayupo pichani). 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akitoa ufafanuzi masuala mbali mbali kuhusiana na semina hiyo.
Ufunguzi wa Semina ukiendelea 
Wakiwa katika picha ya pamoja. 


No comments: