Mchimbaji mdogo wa Madini ya Almas ambaye pia ni Mshauri Mwelekezi wa SANA Gems Gregory Kibusi, akiangalia ubora wa Madini ya Alams.
Na Asteria Muhozya, Arusha
Wachimbaji wadogo wa Madini walioshiriki Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya
Madini ya Vito, Arusha wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ya
uchimbaji bora na uhifadhi wa mazingira kwa wachimbaji nchini.
Ombi hilo lilitolewa na Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya SANA Gems,
ambaye pia ni mchimbaji mdogo wa madini ya Almas, Gregory Kibusi.
Kampuni ya SANA Gems inayofanya shughuli zake za uchimbaji mkoani
Shinyanga ndiyo kampuni pekee ya wachimbaji wadogo iliyokuwa
ikionesha madini ya Almas katika Maonesho hayo.
Kibusi aliongeza kuwa, ushiriki wa wachimbaji katika maonesho hayo ni
fursa kwao ya kukutana na wanunuzi na kujenga mtandao wa kibiashara
hivyo kuiomba serikali kuendelea kuwahamisha wachimbaji wadogo nchini
kushiriki katika maonesho hayo kwa kuwa, yanawezesha uhakika wa
masoko ya madini yao.
"Nikiwa pia kama Katibu Mkuu wa wachimbaji wadogo Shinyanga, natoa
wito kwa wachimbaji nchini kutumia vyama vyao washiriki maonesho haya
ya Arusha kwa kuleta madini yao. Soko la uhakika lipo," alisema Kibusi.
Aidha, Kibusi alitumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji nchini kuachana na
matumizi ya zebaki na kuwataka kutumia njia bora zinazoelekezwa na
Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ravi Hasmukh, alisema
kuwa, kampuni hiyo imeshiriki Maonesho hayo ili kuweza kujenga mtandao
wa kibiashara ikiwemo pia kutoa fursa kwa Watanzania kujifunza namna
Madini ya Almas yanavyochimbwa na mahali yanapopatikana.
Aidha, ameitaka Serikali ifikishe umeme katika eneo hilo na maeneo
mengine mbapo shughuli za uchimbaji mdogo zipofanyika ili kuwezesha
kuharakisha maendeleo ikiwemo kuwezesha shughuli za kiuchumi na
kupanua wigo wa ajira.
Akizungumzia namna kampuni hiyo inavyosaidia eneo linalozunguka mgodi
wake alisema kuwa, kampuni hiyo imetengeneza kisima cha maji kwa ajili
ya kijiji cha Hukiro pamoja na kuboresha baadhi ya miundombinu katika
zahanati iliyo jirani na mgodi wa kampuni hiyo
Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito Arusha yalifunguliwa rasmi tarehe 3
Mei na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Bendera na kufungwa na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Mshauri Mwelekezi wa SANA Gems Gregory Kibusi, (kulia), akionesha
madini ya Almas . Katikati ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ravi Hasmukh.
Kulia ni Mkurugenzi Mwenza Kishan Bhatti.
Madini ya Almas ambayo bado hayajasanifiwa.
Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini ya Almas (TANSORT) kutoka Wizara ya Nishati na Madini Archard Kalugendo (kulia) akimwonesha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (kushoto) namna ya kupima ubora wa Madini ya Tanzanite.
Mjiolojia kutoka Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Jumanne Shimba,
akiangalia madini kwa kutumia kifaa maalum cha kinachotumiwa na kituo
hicho katika mafunzo.
Mnunuzi wa Madini ya Tanzanite (kushoto) akiangalia ubora wa Madini ya
Tanzanite katika Banda la Kampuni ya TanzaniteOne. Kulia ni Mwakilishi
wa Kampuni ya TanzaniteOne.
Watumishi kutoka Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC), wakimsikiliza
mgeni aliyembelea banda la kituo hicho ili kujua shughuli za mafunzo ya
usanifu na unga'rishaji wa madini zinavyofanyika. Mikufu inayoonekana
katika picha pamoja na mapambo mengine imetengenezwa kituo hapo.
Kituo hicho kiko chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Ujenzi wa kisima cha maji kilichojengwa na Kampuni ya SANA Gems Ltd
ikiwa ni sehemu ya kuwezesha jamii inayozunguka mgodi wa kampuni hiyo
kunufaika na uwepo wa mgodi husika.
No comments:
Post a Comment