SHIRIKA la Trust Care Tanzania Foundation kwa
kushirikiana na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wameandaa semina ya kuwajengea
uwezo wa kifikra wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali vya jijini Dar es Salaam
ikiwa na lengo la kuwabadili wanafunzi kwa ujumla kuwa na mawazo chanya
yatakayowawezesha kutumia fursa anuai zinazowazunguka katika jamii mara baada
ya masomo yao.
Akizungumzia semina hiyo inayotarajiwa kufanyika Jumamosi ya
tarehe 20/05/2017 katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam
(DUCE) kuanzia majira ya saa tatu asubuhi, Mkurugenzi Mtendaji wa Trust Care
Tanzania Foundation, Zambert Mbwafu alisema semina hiyo ni maalum kwa wanafunzi
waliopo vyuoni kwa ajili ya kuwajengea uwezo.Alizitaja mada ambazo wanafunzi
wanatarajia kufundishwa ni pamoja na Umuhimu wa Kujiamini na Kujijengea Uwezo,
Uwezo wa Uthubutu, Vipaji na Jinsi ya Kuviendeleza, Maadili na Nidhamu katika
Kazi na Ubunifu katika Kufikia Malengo. “Semina inawaandaa vijana waliopo na
ambao wanatarajia kumaliza elimu yao ya juu hivi karibuni kupata elimu na ujuzi
utakaowasaidia wakiwa shule na baada ya kumaliza masomo yao ili waweze kwenda
sambamba na mahitaji ya ulimwengu wa sasa…” alisema Bw. Mbwafu.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi, Zambert Mbwafu, alivitaja vyuo
vitakavyoshiriki katika semina hiyo; ni pamoja IFM, CBE, DIT, DUCE, TIA, UDSM,
MUHAS, CHUO CHA DIPLOMASIA, KIU, CHUO CHA USTAWI WA JAMII NA CHUO KIKUU CHA
TUMAINI.
Kwa upande wa wadhamini wakuu wa semina hiyo Kampuni ya TTCL,
Injinia Enocent Msasi Mkurugenzi wa Biashara TTCL alisema kampuni hiyo inaunga
mkono kampuni ya Trust Care Tanzania kwa dhumuni lake la kuisaidia jamii katika
maeneo mbalimbali, ikiwemo sekta za kiafya, kielimu na kijamii. Aliongeza kuwa
lengo hilo linashabihiana na lengo la TTCL kuhakikisha inakuwa na jamii bora
zaidi kiteknolojia, kielimu, kiafya na kimaendeleo kwa ujumla.
“TTCL imedhamini semina hii kwasababu inatoa mchango mkubwa katika
kujenga taifa lenye vijana wachapakazi, vijana wenye mtizamo chanya, vijana
wenye uwezo wa uthubutu, na kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha, ”
alisema Msasi na kuongeza kuwa TTCL kupitia huduma zake bora za intaneti, sauti
na SMS inawaunga mkono vijana mara zote na itakuwa mstari wa mbele kufanikisha
juhudi zao za kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“TTCL kwa miaka mingi tumekuwa tukipokea vijana wanaokuja kufanya
mafunzo kwa vitendo kutoka vyuo na taasisi mbalimbali za elimu zinazotoa elimu
katika fani tofauti tofauti. Lakini safari hii tumekuja kivingine zaidi, kwa
kuja na programu ambayo itasaidia vijana kupata uzoefu baada ya kumaliza masomo
yao. Hii itasaidia kuondoa changamoto ya vijana wetu waliomaliza elimu ya juu ambao
mara nyingi hupoteza fursa mbalimbali za ajira kwa kukosa sifa ya uzoefu.”
Vijana watakao pata fursa ya kufanya kazi na TTCL watajifunza
mengi kawa vitendo huku wakiongozwa kwa wataalamu wabobezi katika fani
mbalimbali. Tunaamini watakapomaliza programu hiyo vijana hao watapata fursa
kupata ajira kwenye taasisi na makampuni mbalimbali, au kujiajiri wenyewe,”
alisisitiza Enocent Msasi akizungumza na wanahabari leo.
No comments:
Post a Comment