Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu
kwa Mlipa Kodi wa TRA, Gabriel Mwangosi akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) kuhusu semina juu ya Kodi, Utaratibu na Sheria
kwa wafanyabiashara kutoka China iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika leo Jijini Dar
es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Mrakibu wa uhamiaji na Afisa
Vibali vya Ukazi, Eliud Ikomba akitoa semina kwa wafanyabiashara kutoka
China (hawapo pichani) juu ya sheria za uhamiaji katika semina
iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy
Ltd na kufanyika leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya
Taifa.
Baadhi ya wafanyabiashara kutoka
China wanaofanya biashara zao nchini wakisikiliza mafunzo mbalimbali juu
ya Kodi, Utaratibu na Sheria katika semina iliyoandaliwa kwa
ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika
leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imetoa somo la masuala ya kodi kwa wafanyabiashara kutoka China
wanaoishi nchini kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya sheria na
taratibu za ulipaji kodi katika semina kuhusu mafunzo hayo leo Jijini
Dar es Salaam.
Akiwasilisha mada wakati wa
mafunzo hayo, Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA,
Gabriel Mwangosi amesema kuwa Tanzania ya sasa ina fursa nyingi za
uwekezaji hivyo wafanyabiashara hao watakapokuja kuwekeza lazima
wafahamu kanuni na taratibu za ulipaji kodi nchini ili waweze kuendana
na sheria zilizopangwa na nchini.
“Semina hii mahususi imeandaliwa
kwa ajili ya wafanyabiashara wa kichina wanaoishi nchini kupata mafunzo
ya kodi zikiwemo za zuio, majengo pamoja na ushuru na forodha ambazo ni
lazima wazifahamu kwa manufaa ya Taifa letu na wao pia,”alisema
Mwangosi.
Mwangosi ameongeza kuwa hii ni
mara ya 6 kufanyika kwa semina hizo kwa wafanyabiashara hao ambapo tangu
zianze kufanyika zimewasaidia kutokwenda kinyume na taratibu
zilizowekwa nchini.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa
Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Dotto Stanley amesema kuelimisha umma hasa kwa wageni kutoka nje
ya nchi ni jambo la msingi litakalowarahisishia kufahamu sheria za nchi
ambapo kwa namna nyingine itachochea uwekezaji.
“Kwa kawaida wafanyabiashara
wakubwa huwa wanahitaji kufahamu sheria na taratibu za nchi husika kabla
hawajaamua kuwekeza mahali hivyo mafunzo hayo yatachochea uwekezaji
nchini kwa sababu watakuwa na uelewa wa mchakato mzima juu ya sheria za
uwekezaji na kodi.”alisema Stanley.
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji
kutoka Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd, Anne Werema Maneno amesema
kuwa changamoto kubwa inayowapata wafanyabiashara wa kichina ni kukosa
uelewa juu ya jinsi ya kuwekeza nchini hasa katika suala la ulipaji
kodi.
“Changamoto hiyo inawapelekea
wafanyabiashara kukosa muelekeo wa biashara waliyopanga kufanya kwani
wengi wao wakifika Tanzania hubadilisha biashara baada ya kufahamishwa
sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu biashara hivyo semina hiyo
itawapa uelewa utakaowawezesha kuchagua biashara watakayoweza kuifanya
kulingana na mtaji wa mfanyabiashara husika,”alisema Bi. Anne.
Aidha, katika semina hiyo ya siku
moja imeambatana na fursa ya kupata mafunzo kutoka kwa taasisi zingine
zinazofanya kazi moja kwa moja katika shughuli ya uwekezaji ambazo ni
pamoja na TRA, TIC, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi pamoja na Taasisi
za Kibenki.
Mafunzo hayo juu ya Kodi,
Utaratibu na Sheria kwa wafanyabiashara hao yameandaliwa kwa ushirikiano
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika katika ukumbi
wa Makumbusho ya Taifa ikiwa ni utaratibu wa kawaida wakukutana na wadau
mbalimbali wa Kodi.
No comments:
Post a Comment