Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bibi. Graceana Shirima akiongea wakati wa hafla ya makabidhiano ya mkataba wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu ya Jijini Dar es Salaam unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ufadhili wa TEA.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bw. Msongela Palela akizungumzia faida zinazotokana na mradi wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu ya Jijini Dar es Salaam unaofanywa na shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bibi. Graceana Shirima akimkabidhi mkataba wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Uendelezaji Miliki NHC Bw. Hassan Mohamed, ukarabati huo unafanywa na Shirika la Nyumba la Taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bibi. Graceana Shirima akiwaongoza wadau walioshiriki hafla ya makabidhiano ya mkataba wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu ya Jijini Dar es Salaam unaofanywa na shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukagua baadhi ya majengo na miundo mbinu ya shule hiyo itakayofanyiwa ukarabati.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu Bw. Jovinus Mutabuzi akishukuru Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa kuamua kukarabati miundo mbinu ya Shule hiyo ili kukuza kiwango cha elimu. Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Msongela Palela
Baadhi ya Majengo ya Shule ya Sekondari Pugu yatakayofanyiwa ukarabati na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na yatagharimu zaidi ya milioni mia tisa. (Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo).
Na Fatma Salum- MAELEZO
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeanza rasmi utekelezaji wa mradi wa kukarabati Shule ya Sekondari Pugu iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mkataba wa ujenzi kwa Mkandarasi wa mradi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bibi. Graceana Shirima alieleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 984 zitatumika katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule hiyo.
“Awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule hii itaanza tarehe 1 Juni, 2017 na itafanyika kwa muda wa miezi minne. Ukarabati katika awamu hii utahusisha madarasa, vyoo kwa ajili ya wanafunzi walemavu, mabweni, jengo la utawala, mifumo ya TEHAMA, mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na mifumo ya umeme”alifafanua Bibi. Shirima.
Alieleza kuwa zoezi hilo la ukarabati lilitanguliwa na upembuzi yakinifu wa kubaini hali halisi ya mahitaji ya ukarabati na kazi hiyo ilifanywa na Mtaalamu Elekezi (Consultant).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bw. Msongela Palela alipongeza jitihada za TEA za kukarabati miundombinu ya elimu hasa kwa shule kongwe za Sekondari nchini kote mradi ambao utasaidia kuboresha elimu na kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
“Manispaa ya Ilala inaahidi kushirikiana na TEA na uongozi wa Sekondari ya Pugu kutekeleza zoezi hili na kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.” alisema Palela.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu Bw. Jovinus Mutabuzi alieleza kuwa shule hiyo ina historia kubwa katika nchi yetu na kuishukuru Serikali kupitia TEA kwa ukarabati huo utakaosaidia kurudisha shule hiyo katika hali yake ya awali.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeazimia kukarabati jumla ya shule kongwe za Sekondari 17 ikiwemo shule ya Sekondari Pugu na zoezi hilo limeshaanza kwa shule za Sekondari Nganza, Same na Ilboru.
No comments:
Post a Comment