Monday, May 22, 2017

TASAF NA WADAU WA MAENDELEO WAKUTANA MJINI DSM.


NA ESTOM SANGA-TASAF.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- na wadau wa maendeleo wameanza mkutano wa kutathimini utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa kipindi cha miezi SITA iliyopita.

Mkutano huo unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za TASAF mjini Dar es salaam pia unawajumuisha maafisa wa serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar,pamoja na mambo mengine umefahamishwa juu ya mafanikio na changamoto zilizopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini kwa kipindi cha kuishia mwezi Marchi mwaka huu.

Katika mawasilisho ya shughuli zilizotekelezwa na TASAF katika kipindi kilichopita, imeonyeshwa kuwa zaidi ya kaya milioni MOJA za walengwa zimeendelea kunufaika na Mpango kupitia ruzuku na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoibuliwa na walengwa kupitia utaratibu wa ajira ya muda ambapo hulipwa ujira baada ya kutekeleza kazi hizo.

Aidha taarifa hiyo imeonyesha kuwa kumekuwa na mwitikio chanya wa walengwa katika kuanzisha shughuli za kiuchumi kwa kutumia fedha zinazotolewa na TASAF chini ya utaratibu wa uhawilishaji fedha, na hivyo kusaidia kwa kiwango kikubwa ongezeko la kipato kwa kaya zilizoandikishwa kwenye Mpango.

Mafanikio mengine yaliyoonyeshwa ni ongezeko la mahudhurio ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kutoka katika kaya za walengwa kupata huduma za kliniki kwa lengo la kuboresha afya na makuzi yao pamoja na kuongezeka kwa mahudhurio shuleni kwa watoto wanaotoka kwenye kaya za walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini.

Katika kuboresha zaidi huduma kwa walengwa, TASAF kwa kushirikiana na idara nyingine za serikali imeandaa utaratibu wa kuanza kutoa ruzuku ya fedha kwa njia ya kielektroniki ambapo majaribio yataanza katika baadhi ya maeneo ya Utekelezaji wa Mpango huo.

Wadau hao wa Maendeleo baada ya kuhudhuria mkutano huo wa siku moja watapata fursa ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango huko Zanzibar,Itirima,Magu,Lindi Longido ambako watawatembelea walengwa wa Mpango kuona namna wanaoendelea kunufaika na fedha zinazotolewa katika jitihada za serikali kupitia TASAF katika kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.

Zifuatazo ni picha za washiriki wa mkutano huo wa wadau wa maendeleo ,baadhi ya maafisa wa serikali na watumishi wa TASAF unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo kwenye ukumbi wa mikutano wa Mfuko huo jijini Dar es salaam. 


Msimamizi wa shughuli za TASAF (Benki ya Dunia) Bwana Muderis Mohamed (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo na TASAF .
Baadhi ya wadau wa Maendeleo na Maafisa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF – wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa Mfuko huo katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa maendeleo na TASAF (picha ya juu na chini ) wakiwa kwenye mkutano ulioanza leo kujadili utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya masikini.

No comments: