Monday, May 8, 2017

Tanzania na Afrika Kusini za dhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Tume ya Marais ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 
Sehemu ya Makatibu Wakuu nao wakifuatilia kwa makini Hotuba ya ufunguzi iliyokuwa ikitolewa na Dkt. Mlima.
Dkt. Mlima akiendelea kuzungumza 
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward XolisaMakaya naye akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo. 
Dkt. Mlima pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (wa kwanza kulia), wakimsikiliza kwa makini Bw. Makaya (hayupo pichani). 
Sehemu nyingine ya Maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa Mkutano huo. 
Sehemu ya washiriki kutoka Tanzania na Afrika Kusini walioshiriki katika ufunguzi huo wakiendelea kuwasikiliza viongozi (hawapo pichani)walikuwa wakitoa hotuba zao wakati wa ufunguzi huo. 
Wakiwa katika picha ya pamoja, mara baada ya kumaliza ufunguzi. 
Dkt. Mlima akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ufunguzi. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akielezea jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo kukamilika. 





Tanzania na Afrika Kusini za dhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.


Wataalamu wa Tanzania na Afrika Kusini wapo katika mkutano wa siku nne wa kuandaa mpango bora wa kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi hizo.

Mkutano huo unaojulikana kama Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) umefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima jijini Dar Es Salaam leo.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa kuwa licha ya nchi zetu kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri tokea enzi za ubaguzi wa rangi, lakini bado utakuwa chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo tutakayokubaliana na wenzetu” Balozi Mlima alisema. 

Balozi Mlima alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini BNC ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC. Tokea uwekaji saini wa makubaliano hayo, chombo hicho hakikuweza kukutana licha ya kuwa, makubaliano hayo ndiyo yatakuwa mwongozo katika majadiliano yatakayoendelea hadi tarehe 11 Mei 2017.

Kwa mujibu wa Balozi Mlima, uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda. Kwa takwimu zilizopo takribani makampuni 226 ya Afrika Kusini yamewekeza nchini mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 803.15 na kuajiri zaidi ya watu 20,917. Alisema idadi ya makampuni inaweza kuongezeka kwani kuna makampuni mengi mapya kutoka Afrika Kusini yameshaonesha dhamira ya kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward Makaya alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini hazijafanya vya kutosha kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kijamii. Alisema hadi wakati huu nchi hizo zimesaini makubaliano na mikataba takribani 14 ambayo ni michache ukilinganisha na urafiki na udugu uliopo baina ya nchi hizo. 

Hivyo, alisistiza umuhimu wa kikao hicho kufanya majadiliano yatakayowezesha uwekaji saini wa mikataba mingi zaidi. Alisisitiza umuhimu wa mikataba hiyo kuzingatia maslahi ya pande zote. 


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam, 08 Mei, 2017

No comments: