Thursday, May 18, 2017

SERIKALI YATOLEA UFAFANUZI KAZI YA OFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI

Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imeeleza kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kumuhusisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ukaguzi wa Balozi au ukaguzi wowote ule kama Umoja wa Mataifa kwa sababu hakuna ulazima wa kufanya hivyo Kikatiba na Kisheria.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kiwengwa Khamisi Mtwana Ally (CCM), aliyetaka kujua ni mara ngapi Ofisi hiyo ya Bara imeishirikisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Zanzibar.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, Ofisi hizo kila moja ina mipaka yake ya kufanya ukaguzi na kwamba jukumu la ukaguzi wa Taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kwamba majukumu ya Ofisi hiyo yameainishwa katika ibara ya 143(2) ya katiba hiyo”. Alisema Dkt. Kijaji

Dkt Kijaji aliongeza kuwa, eneo hilo linamtaka Mdhibiti na Makguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka na kutoa taarifa kuhusu ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Bunge na Mahakama.

Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa majukumu hayo yameainishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake za mwaka 2009.

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa, ukaguzi wa Balozi unafanyika chini ya fungu 34, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwa Ofisi zote za Ubalozi ni sehemu ya fungu 34.

“Hivyo basi, ukaguzi wa Balozi kama ilivyo kwa Taasisi nyingine za Muungano unafanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .”alisema Dkt. Kijaji

Aliongeza kuwa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar, majukumu yake yameainishwa kwenye ibara ya 112 ya Katiba (3) ya katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Akiongeza majibu ya swali hilo, Waziri wa Mazingira na Muungano, Januari Makamba alisema kuwa wakaguzi wa pande zote kutoka Tanzania Bara na Visiwani hufanya kazi kwa kushirikiana katika mambo ya ukaguzi wa hesabu za serikali.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Mkwajuni, Ally Zubeir Ngwali (CUF), alihoji ni kwanini fedha za mfuko wa Jimbo hazijawahi kukaguliwa na zitakaguliwa kwa utaratibu upi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo alisema upo utaratibu maalum wa kushughulikia mambo hayo. 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Ashatu Kijaji

No comments: