Friday, May 26, 2017

RC TABORA AHAKIKISHA ULINZI KWA WACHIMBAJI WADOGO WADOGO WANAOFICHUA MAOUVU YA KAMPUNI.

Na Tiganya Vincent

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amesema wachimbaji wadogo wadogo waliofichua maovu yanayofanywa na Watendaji wa Ofisi ya Madini kwa kushirikiana na Kampuni zilizopewa leseni za kuchimba madini katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge wasiwe na wasiwasi kwani Serikali itawashika mkono ili wasidhurike.

Bw. Mwanri alitoa kauli hiyo jana katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge kwenye Mkutano wa hadhara uliowahusisha wachimbaji wadogo wadogo , Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Sikonge na viongozi wa Kampuni zenye leseni ya uchimbaji wa madini kufuatia malalamiko kuwa wachimbaji hao wanaosema ukweli wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa wamiliki wa migodi na baadhi ya watendaji.

Alisema kuwa wamesema ukweli na kufichua maovu yanayoendelea katika eneo la machimbo hayo, Serikali inawahakikishia ulinzi wa kuhakikisha kuwa hakuna mtu yoyote atayenyanyaswa kwa kufichua uovu unafanywa na Kampuni za Uchimbaji Madini katika eneo hilo.


Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Sikonge washirikiane na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Sikonge kuhakikisha kuwa vijana wote walieleza uovu wa watendaji wa Ofisi ya Madini ya Mkoa kwa kushirikiana na Kampuni za madini wanakuwa salama na kuendelea na kazi zao.

Alisema kuwa kiongozi yoyote awe wa Serikali au Kampuni ya Madini asijaribu kuwagusa vijana wote walioeleza matatizo mbalimbali yanayowakabili vingine atakayewagusa atakuwa anakosa sifa za kuendelea kuwa mtumishi wa umma au kuendelea na kazi zake za uchimbaji madini.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Serikali hii iko makini inataka kila mtu au Kampuni itekeleza wajibu wake kama ni kulipa kodi za Serikali ilipe na sio kuendesha shughuli zake kiujanjanja tu na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

Mmoja wa Mchimbaji Wadogo wadogo wa Madini katika eneo hilo la Kitunda Bw. Linus Saidi alisema kuwa Kampuni ya Kapumpa Gold Mining imekuwa ikiwanyanyasa wachimbaji madini wanaonekana kutetea haki za wenzao na kufichua maovu yanayoendelea katika eneo hilo kwa kuwafukuza na kuyafukia mashimo yao.

Alisema uovu mwingine unaendelea ni Kampuni ya Kapumpa kufukua mashimo(maduara) yaliyokataliwa na Serikali kwa hofu za usalama wa wachimbaji wadogo wadogo na kuendelea uzalishaji wakati viongozi hao katika eneo hilo na pindi wanaposikia wanakuja wafurika kwa kuweka majani na miti ili yaonekana kama hayafanyikazi.

Saidi aliongeza kuwa viongozi wa Kampuni ya Kapumpa wamekuwa wakiwadhulumu wachimbaji wadogo wadogo ambao mashimo yao yameonekana kuwa na uzalishaji mzuri na kuwafukuza au kuwakataza kuingia katika eneo la mgodi.

Kwa upande wa mchimbaji madini mwingine Simon Chacha alisema kuwa baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Madini Mkoa wa Tabora wamekuwa wakishirikiana na Kampuni ya Kapumpa katika kuwakandamiza wananchi na kutorosha mapato ya serikali kwa kutoa taarifa zisizo halisi za kiwango cha dhahabu iliyozalishwa.

Aliongeza kuwa mmoja wa watendaji wa Ofisi ya Madini ameongezwa kuwa Mwanahisa wa Kampuni ya Kapumpa , hatua inayosababisha kuficha takwimu za uzalishaji.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa huyo ameahidi kuzifuatilia tuhuma hizo na ikibainika ni kweli kila atachukuliwa hatua kulinga na alivyohusika kwenye tuhuma mbalimbali zilizotajwa.Aliwaomba vijana hao kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati itakapokuwa ikiendelea kufuatilia tuhuma mbalimbali zilizoelewa .

No comments: