Monday, May 22, 2017

MTULE AMCOS WAJIPANGA KUCHANGAMKIA FURSA ZA TADB

 Katibu wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Masoko cha Mtule (Mtule AMCOS), Bw. Ali Fadhil Ali akiongea wakati Benki ya Kilimo ilipotembelea Kijiji cha Mtule kukagua miradi ya kilimo inayohitaji mikopo.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akizungumza na wanachama wa  Mtule AMCOS (hawapo pichani) kuhusu dhima ya Benki ya Kilimo kuwapatia mikopo nafuu wakulima nchini. Kushoto  ni Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo na Afisa Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Bw. Nassor Mohammed (katikati).
 Wanachama wanawake wa Mtule AMCOS wakifuatilia mawasilisho ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB (hayupo pichani) kuhusu uwepo wa mikopo nafuu kutoka Benki hiyo.
 Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha (kulia) akizungumza kuhusiana na mikopo na huduma zinazotolewa na TADB katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Chama cha Ushirika cha Msingi cha Masoko cha Mtule.
 Mwenyekiti wa Mtule AMCOS, Mzee Mgana Zidi Khamis (kulia) akiwaonesha eneo linaloendelezwa la Chama chao linalojengwa kwa michango wa wanachama. Alioongozana nao ni Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (katikati).
 Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo (kushoto) akitoa ushauri kwa Mwenyekiti wa Mtule AMCOS, Mzee Mgana Zidi Khamis (kulia) kuhusu uendelezaji wa miundombinu ya Ofisi ya Chama.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (katikati) akihimiza jambo baada ya kuoneshwa miundombinu ya Ofisi ya Chama cha Mtule AMCOS. Pichani ni Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo (kushoto) na Mwenyekiti wa Mtule AMCOS, Mzee Mgana Zidi Khamis (kulia).
Ugeni wa Benki ya Kilimo wakiwa katika ya pamoja na wanachama wa  Mtule AMCOS.

Na mwandishi wetu, Zanzibar.

Chama cha Ushirika cha Msingi cha Masoko cha Mtule (Mtule AMCOS) kinachojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda  kimeweka bayana nia yake ya kuchangamkia fursa za mikopo nafuu inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuwasaidia katika kuendeleza kilimo chao.

Akizungumza wakati ugeni kutoka TADB ulipotembelea kijijini Mtule, Mwenyekiti wa Mtule AMCOS, Mzee Mgana Zidi Khamis amesema kuwa Chama chake kimejidhatiti katika kufikia soko kubwa la matunda na mboga mboga ila wanarudishwa nyuma na uduni wa mtaji pamoja miundombinu ya masoko.

“Tulisikia uwepo wa Benki ya Kilimo ila hatukuwa tunajua namna ya kuwapa, leo tunaamini kuja kwenu kijiji hapa kumefufua matumaini yetu ya kupatiwa mikopo ili kuongeza tija kilimo chetu na kipato chetu kwa ujumla,” alisema.

Akiwasilisha malengo ya safari yao na umuhimu wa Benki hiyo kwa wakulima nchini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika  kilimo nchini.

Bw. Assenga aliongeza kuwa kilimo cha mbogamboga na matunda  ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa mbogamboga na matunda  nchini.

Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa kilimo cha mazao yote yatokanayo na mbogamboga na matunda  ili kuongeza tija kwa wakulima nchini kote.

 “Benki inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili ya uongezaji tija wa kilimo cha mboga mboga na matunda, uongezaji wa thamani wa mazao ya mboga mboga na mtunda ili kuchagiza uongezaji wa kipato kwa mkulima,” alisema.

Naye, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).

“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” alisema.

No comments: