Saturday, May 20, 2017

Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata) walalamikia ushuru wa mazao


Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Manyara, Mhandisi Munis Weransari akifungua warsha ya matumizi sahihi ya vipimo kwenye mazao iliyoandaliwa na Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata) na kufanyika mjini Babati

Katibu Tawala Msaidizi Mkoani Manyara, (Huduma za Uchumi na Uzalishaji) Felix Mwasenga akifunga warsha ya matumizi sahihi ya vipimo kwenye mazao iliyoandaliwa na Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata) na kufanyika mjini Babati .
……………………………………………………………………………………..

Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata), umelalamikia tozo, ushuru wa masoko na tozo za kusafirisha kwa gunia badala ya kutozwa kwa uzito, kwani hujenga mazingira shawishi kwa wanunuzi na madalali kuzidisha uzito wa vifungashi zaidi ya kiwango stahiki.

Mratibu wa Mviwata mkoani Manyara, Martin Pius alisema hayo mjini Babati kwenye warsha ya uboreshaji matumizi ya vipimo na kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo na matumizi ya mizani wakati wa kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Pius alisema lengo lao ni kutafuta hatua za pamoja kwenye kuboresha biashara ya mazao ya kilimo kwa kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo ili kuongeza tija kwa wakulima, wanunuzi na halmashauri kwa ujumla.

Alisema inatakiwa kuandaa mpango wa pamoja unaotekelezeka kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya vipimo katika wilaya ya Babati na kupashana habari ya maboresho katika sheria ya vipimo, kanuni zake na marekebisho yaliyofanywa.

“Matumizi sahihi ya vipimo ni muhimu sana katika kuhakikisha uwazi na uhakika wa vipimo vinavyotumika, ili wazalishaji, wanunuzi na watumiaji walindwe na serikali ikusanye mapato inayostahili na takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo zipatikane,” alisema.

Alisema tafiti zinaonyesha ukosefu wa uelewa kuhusu vipimo sahihi siyo kwa wakulima au wanunuzi tu bali hata kwa watumishi wa umma ambao wana dhamana kubwa katika kusimamia utekelezaji wake.

Alisema mazoea ya kufanya biashara ya mazao ya kilimo bila kutumia vipimo sahihi yapo kila mahali na kimsingi, biashara ya mazao ya kilimo inayofanyika mashambani hufanywa bila kuhusika kwa wakala wa vipimo.

Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Weransari Munisi alisema ni vyema kutambua pia kuwa sio uzito tu wenye shida katika biashara hii, bali hata vipimo vinavyotumika vinatofautiana kutoka eneo moja na eneo jingine.

Alisema warsha hiyo ni ya muhimu kutokana na mkazo unaowekwa na serikali kuzingatia vipimo sahihi vya ujazo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mizani wakati wa kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

“Ni matazamio yangu kuwa wakala wa vipimo watajenga uelewa wa kutosha kuhusu sheria husika na vipimo stahili kwa mazao ya kilimo na utajenga mtandao wa washirika kudhibiti matumizi ya vipimo visivyo sahihi,” alisema Munisi.

Alisema uuzaji wa mazao mabichi shambani ni kosa na hasara kubwa kwa wakulima kwani huwa hakuna kipimo cha kupima mazao yaliyo shambani, na kunmkosesha mkulima mapato makubwa yatakayopatikana na uuzaji wa mazao hayo pindi atakapovuna na kuuza kwa kutumia vipimo sahihi vya ujazo.

No comments: