Sunday, May 21, 2017

MONGELLA AWATAKA WAUMINI WA DINI MBALIMBALI, WATANZANIA KUDUMISHA AMANI

Na Baltazar Mashaka, Mwanza
SERIKALI mkoani  Mwanza imewataka waumini wa madhehebu ya dini mbalimbali humu na kote nchini kudumisha  umoja, mshikamano na utulivu Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani. 
Kauli hiyo ilitolewa juzi (jana) na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella  (wa pili kushoto pichani) wakati wa Maulid iliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani katika Wilaya ya Nyamagana jijini hapa. 
Alisema kuwa dini zote msingi wake ni amani, kusamehe, kuvumiliana na kushirikiana wananchi na waumini wa dini zote wakiyataimiza hayo nchi itaendelea kuwa kisiwa cha amani. 
“Mikusanyiko kama hii inachangia shughuli za serikali maana yanazungumza amani lakini mengine ni shida.Natamani watanzania leo wangeyasikia ama wakiyasikia na kuyachukua haya nchi itakuwa na amani,”alisema Mongella huku akiweka bayana kuwa yeye ni mnazi wa Simba lakini aliwakabidhi Kombe Yanga kwa amani.
Alidai kuwa kazi bado ni kubwa na kinachotakiwa ni kuwapa wananchi moyo kutokana na kauli mbiu ya Maulid hayo kusistiza umoja, utii wa sheria na ushirikiano na kueleza kuwa hata Aya zilizokuwa zikitolewa hapo amekuwa akizisikia hata kwa Mapadri.
Mkuu huyo wa mkoa alisistiza kuwa nchini itaendelea kuwa kisima cha amani na utulivu kama jamii itakuwa tayari kutimiza matakwa ya dini ambayo msingi wake ni amani , kusameheana, kuvumiliana na kushirikiana.
Pia Mongella alisema serikali inaheshimu kazi zinazofanywa na Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na ndicho chombo inachofanya kazi nacho, naitaendelea kushirikiana kwa maendeleo ya mkoa na taifa maana  haitapa shida kutoka kwao licha ya mifumo iliyopo. 
Aidha, Kaimu Mufti wa Tanzania Sheikh Othman Issa Othman  aliwaonya waumini wa dini ya kiislamu kuwa Mungu amewapa mtihani na hivyo wasizitumie simu za kisasa kufanya vitu haramu na kuvifanya siri, ipo siku vitakuwa hadharani.
“Mwaka huu wa Hijiria tujiandae na mfungo mtukufu wa mwezi Ramadhan.Tunaweza kufanya mambo ya ovyo, ili tutambue Mungu katupa mtihani, mtihani huo anataka kufahamu nani anamwoga kwa siri.Tuzitumie vizuri simu za Smart Phone mamana hata tukiweka namba za siri iko siku hayatakuwa siri tena,”alisema kaimu Mufti.
Alisema  mwenyezi Mungu kawapa Maswahaba wake mtihani ili wavuke  na kuwataka wajiandae na mfungo wa mwezi Ramadhan, hivyo wazitumie simu hizo kutengeneza  makundi ya swala za alfajiri ili kukumbushana ya kheri badala yale ya ovyo yasiyompendeza mwenyezi Mungu.
Awali Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Kuendeleza Quraan na Sunna Tanzania (JUQUSUTA) yenye makao yake jijini Mwanza iliyoandaa Maulid hayo , Sheikh Hassan Kabeke alisema kauli mbiu yake ni kujenga maadili mema, amani na utulivu, kupinga vitendo viovu vya uvunjifu wa amani na utii wa sheria bila shuruti.

No comments: