Na. Eliphace Marwa - Maelezo.
RAIS Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ameongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika maziko ya mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Kitwana Kondo.
Mbali na Mwinyi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyofanyika katika makaburi ya Tambaza ni Makamu wa Rais Mstaafu, Mohammed Gharib Bilal, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Salim Ahmed Salim na Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wengine.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mzee Mwinyi alisema, marehemu Kondo alikuwa ni mtu ambaye alijitoa katika kulitumikia taifa kwa moyo wake, hivyo mchango wake ni mkubwa katika kulitumikia taifa na hasa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam.
"Alikuwa ni rafiki yangu ambaye tumefahamiana kwa muda mrefu sana, tumepoteza mtu muhimu sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa, tumuombee kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi," alisema Mzee Mwinyi
Kwa upande wake, Kinana alisema, taifa na hasa wakazi wa Dar es Salaan wamepata pigo kubwa kwa kumpoteza mzee huyo ambaye bado busara zake zilikuwa zikihitajika.
"Alikuwa ni kiongozi wa jamii,alikuwa ni mwalimu wa watu wengi katika manbi mbalimbali, ni msiba mkubwa lakini nj kazi ya Mungu, tuendelee kumuombea apumzike kwa amani," alisema Kinana.
Naye, Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa alisema, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mzee Kondo ni vema uongoziu wa jiji kuangalia namna ambavyo barabara moja ya jiji hilo likapewa jina la KK ikiwa ni kuheshimu na kutambua mchango wake.
"Namuomba Mstahiki Meya, barabara moja uiite KK, itakuwa ni heshima kumuenzi Mzee Kitwana Kondo kwa kazi kubwa aliyofanya wakati wa uhai wake," alisema Lowassa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) , Profesa Ibrahim Lipumba alisema, mchango wa Mzee katika taifa ni mkubwa lakini kwa bahati mbaya ni kama jmeshindwa kutambuliwa.
"Ni mtu ambaye bahati mbaya sana historia ya nchi yetu haitambui mchango wake katika kuleta uhuru wa nchii na kudumisha uhuru wa nchii," alisema Profesa Lipumba.
Akieleza chanzo cha kifo cha baba yake, mtoto wa kwanza wa marehemu Mzee Kondo, Stara Kondo alisema, Baba yake alilazwa katika hospitali ya Hindu Mandal Mei 18 kutokana na kuugua muda mrefu lakini alifariki juzi.
“Alikuwa anaumwa muda mrefu lakini hadi anafariki madaktari walisema alipata stroke (Kiharusi) na shinikizo la damu, tutamkumbuka kwa mambo mengi kwa sababu ni baba lakini alikuwa ni kichwa cha familia,” alisema Stara
Baadhi ya Ndugu Jamaa na Marafiki wakiwa wamebeba Jeneza lenye mwili wa aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Kigamboni na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mzee Kitwana Kondo wakielekea kwenye maziko yake,leo Alhamisi baada ya swala alasiri katika makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam.
Mazishi ya aliyekuwa Meya wa Dar es salaam Mzee Kitwana Kondo jioni hii makaburi ya Tambaza jijini Dar
Mazishi ya aliyekuwa Meya wa Dar es salaam Mzee Kitwana Kondo jioni hii makaburi ya Tambaza jijini Dar
Mwili wa Marehemu Mzee Kitwana Kondo ukiingizwa msikitini kwa ajili ya kuswaliwa tayari kwa mazishi jioni ya leo ,katika Makaburi ya tambaza,jijini Dar.
Ndugu jamaa na marafiki wakiwa Makaburi wakisubiri kuupokea mwili wa Marehemu kwa ajili ya Maziko katika Makaburi ya Tambaza,jijini Dar
No comments:
Post a Comment