Monday, May 8, 2017

KATIBU MKUU WIZARA YA UCHUKUZI, DKT LEONARD CHAMURIHO AKEMEA UDOKOZI NA WIZI KATIKA USAFIRI WA ANGA.

Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Masuala ya Kiuchumi , Mamlaka ya Usafiri wa Anga Dan Malanga (wa kwanza Kushoto) akimsikiliza Meneja wa uwanja wa ndege wa Dodoma, Julius K. Mlungwana,(wa Pili Kushoto) wakati kamati ya kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga ilipotembelea kiwanja cha ndege Dodoma May, 8 2017.
Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Masuala ya Kiuchumi, Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dan Malanga (Amesisima) akisisitiza jambo wakati wa kikao cha 42 cha wajumbe wa kamati ya kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga kilichofanyika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma May, 8 2017.
Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Rogatus Hussein Mativila akifungua kikao cha 42 cha wajumbe wa kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga Kilichofanyika Ukumbi wa Hazina mijini Dodoma May, 8 2017.
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga katika picha ya pamoja wakati wa kikao cha 42 kilichofanyika Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma May, 8 2017.
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga Wakitembelea Vifaa vya Kutolea Huduma za Usafiri wa Anga kama sehemu ya mkutano wao wa 42 uliofanyika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma May, 8 2017.
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga Wakikagua Njia ya Ndege ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma Kama Sehemu ya Mkutano wao wa 42 uliofanyika Ukumbi wa Hazina Dodoma May, 8 2017.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuriho amewakumbusha wadau wa usafiri wa anga kusughulikia na kumaliza tatizo la wizi na udokozi katika usafiri wa anga, hali ambayo amesema inahatarisha usalama na ustawi wa sekta hii hapa nchini.

Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa 42 wa kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Usafiri wa Anga (National Air Transport Facilitation Committee) iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi - Sekta ya Uchukuzi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Rogatus Hussein Mativila, Dkt. Chamuriho ametoa mfano wa taarifa za hivi karibuni katika vyombo vya habari kuhusu wizi wa mafuta ya ndege hali ambayo amesema itajenga hofu kwa watumiaji wa uchukuzi wa anga . 

"Matukio kama haya hayaatarishi usalama tu, lakini pia ustawi wa sekta kwa vile yatajenga hofu kwa wasafiri na kusababisha wachague njia nyingine". Alisema Katibu Mkuu na kuongeza ustawi wa usafiri wa anga katika nchi yoyote, unategemea na upatikanaji wa huduma bora katika viwanja vya ndege, usalama wa abiria na mali zao, ndege na miundombinu mbali mbali .

Amewakumbusha wajumbe wa kamati ya kitaifa ya uwezeshaji usafiri wa anga kujadili suala hilo la udokozi na wizi katika sekta ya usafiri wa anga na kuwataka watoa huduma za usafiri wa anga kuhakikisha, wanatoa huduma kwa haraka , weledi na katika viwango vinavyokubalika kimataifa.

Kamati ya Uwezeshaji wa Masuala ya Usafiri wa anga inajumuisha wajumbe kutoka taasisi mbali mbali zinazojihusisha na kufanikisha usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga(TCAA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege(TAA), Wizara ya Mambo ya Ndani, Utalii, Kilimo, na kampuni zinazotoa huduma za usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kampuni za ndege.

Mkutano huu hufanyika mara mbili kwa mwaka ili kuwezesha wajumbe kubadilishana mawazo na kuangalia namna ya kuboresha Uchukuzi wa anga hapa nchini.

No comments: