Wednesday, May 31, 2017

JAFO AWAONYA WAKANDARASI WA MIRADI YA TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo amewataka wakandarasi wanaojenga miradi ya miundombinu mbalimbali kwenye Halmashauri nchini kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ndani ya muda na inakuwa na ubora unaotakiwa.

Jafo alitoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa mradi wa Maji Wilunze wilayani humo.

Mradi huo umefanikiwa kukamilika na kuzinduliwa rasmi kufuatia maagizo aliyoyatoa Machi,26 mwaka huu baada ya kutembelea na kubaini kuna uzembe Mkubwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Baada ya kubaini hilo, Jafo alitoa kalipio kwa watendaji wa Halmashauri pamoja na Mkandarasi wa ujenzi wa mradi na kuagiza mradi huo ukamilike haraka ifikapo leo Mei 30, mwaka huu, kinyume cha hapo atawachukulia hatua kali watendaji na Mkandarasi endapo angeshindwa kukamilisha ndani ya muda huo.

Aidha, Jafo alimwambia mkandarasi wa Mradi huo kuwa endapo asipotekeleza asitegemee kupata kazi yeyote iliyo chini ya Halmashauri yeyote hapa nchini kwani Ofisi ya Rais Tamisemi haiwezi kuvumilia wakandarasi wazembe. 

Kukamilika kwa mradi huo, kumepokewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Wilunze maarufu kwa jina la Chalinze nyama kwa kuwa awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Akizindua mradi huo, Jafo alisema wakandarasi wengi wamekuwa wababaishaji katika kutekeleza miradi kwa wakati na kuwa kikwazo cha miradi mingi kushindwa kukamilika kwa wakati huku wananchi wakiendelea kupata shida.

Alifafanua kuwa katika awamu hii ya tano hakuna nafasi kwa wakandarasi wababaishaji ambao wamekuwa wakibembelezwa katika kukamilisha miradi ya jamii na kuwaonya kuwa dhama zimebadilika hakuna wakati tena wa kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyokuwa zamani.

Naye, Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Joel Mwaka alimshukuru sana Naibu Waziri kwa umakini mkubwa katika utendaji wake kwa kuwa amekuwa ni kiongozi wa kuigwa hapa nchini.“Mheshimiwa Jafo anafuatilia mambo kwa umakini na kupata matokeo makubwa kwa kila miradi anayo isimamia hapa nchini nimeona hilo mikoa mbalimbali hapa nchini,”alisema Mwaka.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na wananchi wa Wilunze kata ya Manchali katika uzinduzi wa mradi wa maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo pamoja na Mbunge wa Jimbo la Chilonwa Joel Mwaka wakipiga makofi baada ya kuzindua mradi wa maji Wilunze.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa kwenye kigoda cha kigogo huku akiwa amevishwa mgolole na kupewa fimbo ikiwa ni ishara ya shukrani kutoka kwa wananchi baada ya kuwezesha kukamilika mradi wa maji Wilunze.
Jiwe la msingi la Mradi wa maji Wilunze
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza mara baada ya kumtwisha ndoo ya maji mmoja wa wananchi wa kijiji cha Wilunze.

No comments: