Tuesday, May 16, 2017

HALMASHAURI NCHINI ZAKUMBUSHWA WITO WA KUNUNUA DAWA ZA KUUA VILUWILUWI VYA MBU WAENEZAO MALARIA

Jengo la Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria lililozinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn tarehe 2 Julai, 2015 Kibaha, Pwani.
Mtaalam wa Maabara ya Uandaaji Bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Bw. Fumbuka Pauline akiwaeleza Waandishi wa habari baadhi ya kazi wazifanyazo wakati wa kuwaandaa bakteria 15 Mei, 2017. Kushoto ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Bw. Samwel Mziray.
Mmoja wa Waandishi wa Habari (kulia) akipiga picha ya bakteria wanaoonekana kwa kifaa maalum cha kuangalia bakteria (Microscope) katika Maabara ya kuaandaa bakteria 15 Mei, 2017 Kibaha, Mkoani Pwani.
Mtaalam wa Maabara ya Uandaaji bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani akiangalia bakteria kwa kutumia kifaa maalum (Microscope) kabla ya kuwapeleka sehemu inayohusika kwa ajili ya hatua nyingine, 15 Mei, 2017.
Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria, Bw. Samwel Mziray (kulia) akiwaeleza Waandishi wa habari baadhi ya kazi zinazofanywa katika moja ya mitambo iliyopo kiwandani hapo 15 Mei, 2017.
Baadhi ya mitambo iliyopo katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Kaimu Meneja Masoko na Mauzo wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria, Bw. Frank Mzindakaya akiwaeleza Waandishi wa habari (hawapo pichani) namna kiwanda hicho kinavyoandaa madumu ya dawa kwa ajili ya kuyasambaza kwa wateja wake 15 Mei, 2017 Kibaha, Mkoani Pwani.
Mtaalam wa Uthibiti wa Ubora wa Dawa wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria, Dkt. Nicholaus Banzi akiwaelezea Waandishi wa habari namna hatua za ukuaji wa mbu na namna dawa zinazotengenezwa na kiwanda hicho zinavyoweza kuua mazalia ya viluwiluwi vya mbu wa malaria.

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

………………….

Na Benedict Liwenga-WHUSM.

Halmashauri nchini zimetakiwa kuitikia wito wa kununua dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria zilizoanza kuzalishwa hapa nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria cha Tanzania Biotech Products Limited kilichopo Kibaha Mkoani Pwani, Bw. Samwel Mziray wakati alipokutana na Waandishi wa habari na kufanya nao mazungumzo juu ya shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho.

Bw. Mziray amesema kuwa, dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria zinapaswa kununuliwa na kila Halmashauri nchini kwa maagizo yaliyotolewa na Serikali kupitia waraka wake kwa kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kilijengwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kupambana na malaria nchini. Hata hivyo amebainisha kwamba mpaka sasa mwitikio wa halmashauri umekua mdogo kwani ni halmashauri mbili tu za Geita pamoja na Mbogwe ndizo zimeshanunua dawa hizo.

“Lengo la Serikali kuja na mpango huu ni kupunguza vifo vitokanavyo na malaria nchini na kupunguza gharama kubwa ya kununua dawa na vifaa tiba vya kupambana na malaria”, alisema Mziray.

Amesema kwamba iwapo kama halmashauri zitanunua dawa hizo na kuzitumia, ugonjwa huo utapungua kwa kiasi kikubwa nchini na hivyo serikali kuelekeza fedha zake katika shughuli za maendeleo.

Amesema kwamba, kwa Afrika kiwanda hicho ni moja ya kiwanda kilichobahatika kujengwa Tanzania ambapo nia ya Serikali ni kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa kuharibu mazalia ya mbu.

Ameongeza kuwa, kiwanda hiki kitazalisha mbolea ya kibaiolojia (Bio fertilizer) siku za usoni, lakini kwa sasa kiwanda kinazalisha dawa za aina mbili ambazo ni Bactivec na Griselesf ambazo hutumika kwa kunyunyuzia katika mazalia ya mbu.

Amefafanua kwamba, kwa sasa kiwanda hicho kinaweza kuzalisha kwa wingi dawa hizo ambapo ametaja moja ya nchi iliyonunua dawa hizo ni Niger ambayo tayari imenunua lita 91,000 na nchi nyingine za Serbia na Srilanka ziko katika mazungumzo ya kununua dawa hizo.

“Niiombe Serikali iweze kutoa msukumo zaidi kwa halmashauri ambazo bado hazijanunua dawa hizi kukitumia kiwanda hiki kufikia malengo kwani jamii inapoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa wa malaria”, alisema Mziray.

Amefafanua kuwa, dawa hizo zinaweza kutumika katika kipimo cha mililita moja kwa lita 50 za maji na bei ya lita moja ni shilingi 13,000/= na zina uwezo mkubwa wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu wa malaria.

Kuhusu agizo la Serikali la kuzitaka halmashauri nchini kununua dawa hizo amesisitiza kwamba utekelezaji wa halmashauri hizo kuja kiwandani unapaswa kuwekewa kipaumbele na Serikali na halmashauri hazinabudi kuitikia wito huo.

“Serikali imeshatoa waraka kwa halmashauri zote nchini kuweza kutumia kiwanda hiki kununua dawa, kwahiyo sasa kilichobaki ni utekelezajina suala la bei sio kisingizio, suala kubwa ni utayari na kuona umuhimu wa kufikia malengo ya kutokomeza malaria kwa jamii”, alisema Mziray.

Aidha, amebainisha kuwa, jukumu la kununua dawa hizo liko chini ya halmashauri husika na inatakiwa kupanga bajeti yake ya kununua dawa hizo.

Kuhusu suala la usalama wa dawa hizo amesema kwamba, dawa hizo ni salama kwa binadamu na Kiwanda kinafanya mawasiliano na vyombo vya habari ili kutoa elimu na mkazo mkubwa wa kununua dawa hizo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Masoko na Mauzo wa Kiwanda hicho, Bw. Frank Mzindakaya amesema kwamba, Serikali hainabudi kutenga bajeti ya kutosha ili kuziwezesha halmashauri kununua dawa hizo.

Ameongeza kuwa, dawa za kiwanda hicho wanaziweka katika vipimo mbalimbali ikiwemo vya lita 20 na ujazo wa miligramu 30 na katika matumizi makubwa mteja mkubwa ni Serikali yenyewe kwakuwa ndiyo inayonunua kupitia Halmashauri na kwenda kuzinyunyuzia katika madimbwi. Kwa mwananchi wa kawaida anaweza kununua miligramu 30 ili aweze kutumia kwa matumizi ya kifamilia ya kujikinga yeye na familia yake.

“Serikali haijamtwisha mzigo mwananchi yeyote wa kununua dawa hizi ndiyo maana tunazisisitiza kuwa halmashauri zije kununua dawa hizi ili ziende kuwasaidia wananchi kwa kuziweka katika madimbwi makubwa na hatimaye kuwalinda wananchi dhidi ya malaria”, alisema Mzindakaya.

Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) ni Kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo (NDC) iliyopewa dhamana ya kusimamia na kuendesha kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia zikiwemo viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu waenezao malaria (Biolarvicides). Kiwanda hiki kipo eneo la TAMCO Kibaha, Mkoa wa Pwani.

No comments: