Halmashauri za wilaya zimetakiwa kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maji kwa kuchangamkia fursa ya fedha za kitanzania bilioni 250 zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji safi na salama vijijini (2016-2020).
Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Injinia Jackson Mutazamba aliwaambia wakurugenzi wa wilaya katika semina inayofanyika mjini Morogoro jana kuwa ni halmashauri chache tu ndio zimeanza kupata fedha hizi mara baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa na wafadhili.
"Kuna fedha za kutosha katika mradi huu ukilinganisha na mwamko wa halmashauri katika kuchangamkia fursa hii ya kuongeza mtandao wa maji katika maeneo yao," alisema na kuongeza kuwa fedha hizi zinaweza kuzisaidia halmashauri kuanzisha miradi mipya na kukarabati ile ya zamani ili iweze kutoa maji kwa wakati wote wa mwaka.
Alisema moja ya sharti la upatikanaji wa fedha hizi ni ufanisi katika utekelezaji wa miradi iliyopita na ubora wa ripoti za kila mwezi kama ambavyo programu hii inavyozitaka halmashauri. Kigezo hiki ni muhimu sana katika kuvuka hatua moja hadi nyingine na kupata fungu kubwa zaidi la fedha ambalo litawezesha kutekeleza miradi mikubwa zaidi katik halmashauri husika.
Kwa mfano halmashauri zinaweza kupokea aina mbili za malipo kama vile paundi za kiingereza 50 kwa ajili ya kuendeleza kituo cha maji na fungu hili linaweza kuongezeka hadi paundi 1,500 kulingana na ufanisi wa utekelezaji katika hatua ya mwanzo.
"Ukipata paundi zaidi ya 1,500 kwa mara moja kwa miradi ya vijijini ni nyingi sana katika kuiboresha na kuifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wote. Na pia fedha hizi zinaweza kutumika kuanzisha vituo vipya vya kusambazia maji hivyo kufanya mtandao wa maji kuwa mkubwa zaidi katika eneo husika," alisema.
Alisema ni halmashauri 57 tu ambazo ziliweza kuvuka vigezo viwili vya mwanzo kwa mwaka jana na kuweza kupata fungu kubwa zaidi la kiasi cha paundi za uingereza 5,000, fedha ambazo kwa miradi ya maji vijijini zinaweza kusaidia sana katika upatikanaji wa maji wakati wote wa mwaka.
Aliwahimiza wakurugenzi wa wilaya kuchangamkia fursa hii ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi ya maji na kuifufua ile ambayo imekufa ianze kufanya kazi tena na kuongeza mtandao wa maji kuwa mkubwa zaidi ili kufikia adhma ya serikali ya asilimia 95 wa watu wanaopata maji katika miaka michache ijayo.
Injinia Mutazamba aliongeza kusema lengo la kuwakutanisha wakurugenzi wote nchini katika semina hiyo ni kuweza kuwaeleza kwa kina kuhusu fursa hii ya fedha za wafadhili ambazo bado zipo nyingi na zinaweza kusaidia kupunguza na hata kumaliza kabisa tatizo la maji hasa sehemu za vijijini.
Alisema programu hii ya kuongeza mtandao wa maji vijijini unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya shirika la kimataia la DFID la uingereza na serikali ya Tanzania.
Mratibu wa mradi wa usafi wa mazingira uitwao Nipo Tayari Juliana Kitira akimuonyesha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko, Kigoma, Elinatha Elisha takwimu za hali ya usafi wa mazingira katika halmashauri yake kwenye simina inayofanyika Morogoro. Mradi huo pia unahamasisha uwepo wa vyoo bora na kunawa mikono na maji safi baada ya kutoka chooni.
Mkurugenzi wa wilaya ya Bagamoyo Fatuma Latu akiangalia msimamo wa wilaya yake katika usafi wa mazingira kupitia mradi wa Nipo Tayari chini ya Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia, Watoto, Walemavu na Wazee kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Simanjiro mkoani Manyara Yefred Myenzi akiapa kuwa yupo tayari kutekeleza kwa vitendo kampeni ya nchi nzima ya usafi wa mazingira iitwayo Nipo Tayari kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Sabas Damian Chambasi akiapa kuwa yupo tayari kutekeleza kwa vitendo kampeni ya nchi nzima ya usafi wa mazingira iitwayo Nipo Tayari kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment