Wednesday, May 10, 2017

Eckobank Tanzania leo imewahakikishia wateja wake kuendelea na shughuli zake nchini Tanzania


 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Raphael Benedict amefanya mkutano na waandishi wa habari leo katika ofisi za makao makuu ya benki hiyo, na kueleza kwamba hawana dhamira ya kusitisha shughuli zao nchini kutokana na ahadi na malengo makubwa waliyojiwekea ya kuleta maendeleo ya kiuchumi Tanzania.

“Hii ilikuwa ni ahadi yetu tangu tulipoanza kufanya shughuli zetu hapa nchini miaka saba iliyopita na itaendelea kuwa ahadi yetu mpaka hivi sasa,” alisema Benedict.

Licha ya kukiri kwamba kumekuwapo na ongezeko la wateja kushindwa kurejesha mikopo yao mwaka jana, alisema benki hiyo imejiwekea utaratibu mzuri na hatua sahihi za jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Alisema, “Tumechukua hatua muhimu ili kuwezesha urejeshaji wa mikopo mbalimbali ndani ya miezi mitatu iliyopita na tunaamini kwamba mfumo tuliouanzisha utatuletea mafanikio makubwa ndani ya miezi michache ijayo.”

Aliongeza kuwa, nguvu ya msingi ya benki hiyo ina ungwa mkono na wanahisa wakubwa ambao wanaifanya benki kuwa imara, madhubiti na kuaminika na hivyo kuwa moja ya chombo cha fedha kinachoweza kuendana na hali yoyote ya dhoruba.

Washirika wakubwa wa Ecobank ni pamoja na Nedbank ya Afrika Kusini( asilimia 21), Qatar Nation Bank (asilimia 20), Public Investiment Corporation ya Afrika Kusini ( asilimia 14) na International Finance Corporation iliyopo chini ya Benki ya Dunia (asilimia 14).

Benedict aliongeza kwamba Ecobank ina shauku kubwa ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuendeleza uchumi kupitia huduma zake. Hata hivyo, mwaka 2016 ilishuhudia ongezeko la kutokulipwa kwa mikopo, jambo ambalo liliisukuma benki hiyo kubadilisha mbinu na kuja na mikakati mipya ya kukabiliana na hali hiyo.

Alielezea kwamba Ecobank Tanzania haina lengo la kufunga huduma zake na badala yake imeanza kufanya mabadiliko katika shughuli zake ili kuweza kukabiliana na hali ya sasa.

Pia aliongeza kwamba ili kuendelea kuwahudumia wateja wake kwa ufanisi zaidi, benki hiyo imewekeza zaidi kwenye huduma zake za kimtandao na malipo ili kuweza kuwahudumia wateja wake kwa urahisi zaidi na taifa kwa ujumla.

“Hivi karibuni tulizindua app ya Ecobank Mobile Banking ambapo wateja watapata huduma ya Xpress Akaunti.

Huduma ya Xpress Akaunti inawawezesha wateja kufungua na kutumia akaunti zao bila ya kufika kwenye matawi yetu, huku wakiokoa muda, pesa na kuongeza ufanisi na usalama, hii yote ikiwa ni mikakati ya Ecobank kwa Afrika.

Malengo mazuri ya Ecobank ya baadaye ni kuwa taasisi imara iliyojikita kwenye msingi mzuri.

Kwa mara nyingine ninapenda kuwahakikishia tena wateja wetu na wadau kwamba tutaendelea kuwepo hapa.
 


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EcoBank Tanzani Raphael Benedict akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwahakikishia wateja wa benki hiyo na umma wa ujumla kuhusu dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kutoa huduma zake hapa nchini. Kushoto Mkuu wa kitengo cha Wateja wa rejareja wa benki hiyo, Ndabu Lilian Swere.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EcoBank Tanzani Raphael Benedict akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya dhamira ya benki hiyo ya kutositisha shughuli zao nchini kutokana na ahadi na malengo yao. Kulia ni Mkuu wa kitengo cha biashara wa benki hiyo Respige Kimati.
Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa wa EcoBank Tanzania Raphael Onyango akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya dhamira ya benki hiyo ya kutositisha shughuli zake hapa nchini kutokana na ahadi na mikakati madhubuti waliyojiwekea. Wa pili kushoto ni Ndabu Lilian Swere, Mkuu wa kitengo cha Wateja wa rejareja, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EcoBank Tanzania, Raphael Benedict (wa pili kulia) na Mkuu wa kitengo cha biashara wa benki hiyo Respige Kimati (kulia).
Mkuu wa kitengo cha biashara wa Ecobank Tanzania, Respige Kimati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya dhamira ya benki hiyo ya kutositisha shughuli zake nchini kutokana na ahadi na malengo yake. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EcoBank Tanzani Raphael Benedict na kushoto ni Mkuu wa kitengo cha huduma za biashara za ndani Ndabu Lilian Swere.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EcoBank Tanzania, Raphael Benedict, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya dhamira ya benki hiyo ya kutositisha shughuli zake nchini kutokana na ahadi na mikakati waliyojiwekea. Kulia ni Mkuu wa kitengo cha biashara wa benki hiyo Respige Kimati na kushoto ni Ndabu Lilian Swere, Mkuu wa kitengo cha wateja wa rejareja.

No comments: