Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi afisa wa usalama
kutoka shirika la TANESCO Mkoa wa Singida Juma Mauba zawadi ya cheti na TV flat screen baada ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora mwaka 2017.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa ameshikama na Mwenyekiti
wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoa wa Singida Aaran Jumbe
(kulia kwake) na Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (kushoto kwake)
wakiimba wimbo maalumu wa wafanyakazi wa Mshikamano daima pamoja na
wimbo wa taifa.
Watumishi
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku
ya wafanyakazi kwa Mkoa wa Singida.
Watumishi
wa Kutoka Halmashauri ya Ikungi wakipita mbele ya Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi na kuonyeshwa mazao ambayo huzalishwa kwa
wingi wilayani humo ambayo ni viazi vitamu na alizeti katika maadhimisho
ya siku ya wafanyakazi kwa Mkoa kwa Mkoa wa Singida.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akitoa zawadi ya mpira kwa
viongozi wa wafanyakazi wanawake kwa halmashauri zote saba za Mkoa wa
Singida ili waweze kuunda timu za wanawake katika halmashauri zao.
Waajiri
wote Mkoani Singida hususani wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio
wenye watumishi wengi wameelekezwa kujenga mahusiano mazuri baina yao
ili kuboresha utumishi wao.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa maelekezo hayo wakati wa
maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mkoani hapa yaliyofanyika katika
uwanja wa Peolpe’s mjini Singida.
Dkt.
Nchimbi amesema mwajiri na mtumishi sio maadui bali wanapaswa kujenga
mahusiani mazuri hasa kwa mwajiri kujenga mazoea ya kufahamu sifa za
watumishi wake, shida na matatizo yao.
Ameongeza
kuwa waajiri wamekuwa wakisubiria watumishi wakosee ndio wawape adhabu
lakini haipaswi kuwa hivyo kwani mwajiri anatakiwa ahakikishe anaweka
mazingira mazuri na kumuelimisha mtumishi asifanye makosa.
“Ukiona
mtumishi anafanya mambo yanayokinzana na sheria, kanuni na utaratibu,
usimkaripie wala kumtega, mtafutie afisa ustawi wa jamii. Kwa vyo vyote
afisa ustawi wa jamii atamrejesha kwenye mstari stahiki na mambo
yatakwenda vizuri”.
Aidha
Dkt Nchimbi amewataka wakurugenzi kutofanya ziara nyingi nje ya
halmashauri zao bali wajikite katika kusikiliza na kutatua kero za
wananchi na watumishi wao ambazo watazibaini endapo watafanya ziara za
kutosha katika halmashauri zao.
Amesema
ili kuboresha maslahi ya watumishi, waajiri wanapaswa kuandaa mafunzo
kwa watumishi juu ya matumizi bora ya fedha ili waweze kutunza fedha
zao, kila halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya watumishi kupewa
viwanja vya makazi pamoja na kila halmashauri kuwa na afisa ustawi wa
jamii atayehusika na watumishi kwa ajila ya masuala ya ushauri.
Pia
Dkt. Nchimbi amekemea tabia mbaya ya baadhi ya wakuu wa idara/vitengo
ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wafanyakazi wa kike walio chini
yao.
“Wakuu
hawa wa idara/vitengo wanakiuka sheria kanuni na taratibu kwa kuanzisha
mahusiano ya kimapenzi humo humo kazini. Wakati mwingine wanafanya
mapenzi na wake za watu. Tabia hii haikubaliki na haivumiliki hata
kidogo. Viongozi au wakuu wa idara/vitengo wenye tabia ya aina hii,
waiache mara moja”, amesema Dk.Nchimbi.
Kwa
upande wao wananchi na watumishi Mkoani Singida wamempongeza rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake
utumishi wa umma ambapo kwa sasa amerejesha nidhamu na uadilifu kwa
kiwango cha kuridhisha.
Wananchi
hao wamesema chini ya serikali ya awamu ya tano watumishi wa umma
wamebadilika sana na sasa wanatoa huduma kwa ukarimu mkubwa, wepesi na
uharaka zaidi tofauti na ilivyokuwa awali.
“Huko
nyuma watumishi wa umma wengi walikuwa wana urasimu wa hali ya juu.
Walikuwa wakitoa huduma huku macho na akili zao zikiwa kwenye
‘whatsapp’. Mbaya zaidi mwananchi ukipeleka kero zako, wanakuona ni
msumbufu. Hivi sasa mambo ni tofauti kero za wananchi zinatafutiwa
majibu na majawabu kwa wakati,” ameongeza Dkt. Nchimbi akiunga mkono
maoni ya wananchi.
Mmoja
wa wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo Sombi Hangida amekiri kwamba
ni kweli watumishi wa umma wamebadilika mno na sasa wanatoa huduma bila
kuomba rushwa na wamekuwa na lugha rafiki kwa wananchi.
Awali
mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoani Singida
Aaran Jumbe amehimiza kuhusu mabaraza ya wafanyakazi kufanyika katika
maeneo ya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hasa
kuwashirikisha vyama vya wafanyakazi.
Jumbe
ameongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikitoa ushirikiano kwa vyama vya
wafanyakazi na kuomba ushirikiano huo uendelee huku akisisitiza zawadi
za mfanyakazi hodari zinazo ahidiwa na taasisi na halmashauri zitolewe
kwa wakati.
No comments:
Post a Comment