Friday, May 12, 2017

CCM Z’BAR YAWAFARIJI WALIOATHIRIWA NA MAFURIKO.


Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma akipokea maelezo kutoka kwa viongozi wa mtaa akiwemo sheha wa shehia ya Tomondo, Mohamed Omar katika eneo la Ziwa maboga ambapo zaidi ya nyumba 200 zimeathiriwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha. 
Nyumba mbali mbali zilizoathiriwa na maji ya mvua katika eneo la Tomondo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja. 
Nyumba zilizovamiwa na maji katika eneo la Meli nne Makaburini Unguja. 
Katibu wa Tawi la CCM Tomondo, Hassan Kipanga Abdalla akimweleza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar hali ya waakazi wa shehia hiyo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa. 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Abdalla Juma Saadala akiwafariji wananchi wa eneo la Mwanakwerekwe Meli nne, waliopata maafa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa. 
Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala akimfariji mmoja wa wananchi ambaye nyumba yake imeporomoka kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha hivi sasa nchini, uko Fuoni Migombani Zanzibar.

……………………………………..

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

ZAIDI ya Nyumba 300 katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi zimeathiriwa na Mvua za masika zinazoendelea kunyesha hivi sasa.

Akizungumza katika mtaa wa ziwa maboga sheha wa shehia ya Tomondo, Bw. Mohamed Omar Said alisema zaidi ya nyumba 200 katika eneo hilo zimeathiriwa na mvua kwa kujaa maji na zingine kuporomoka.

Bw. Said alifafanua kwamba baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wamehama katika makaazi yao na kuomba hifadhi katika maeneo mengine yaliyokuwa salama, huku idadi ya nyumba zinazoathiriwa na mvua hizo zikiendelea kuongezeka kadri mvua zinavyioendelea kunyenyesha.

Mbali na maeneo hayo pia katika mitaa ya Meli nne, Fuoni janga mizini na Fuoni Migombani kuna nyumba zaidi ya 100 zimeathiriwa na mvua hizo.

Akizungumza juu ya athari hizo, Mjumbe wa sheha wa shehia ya kibondeni, Bi. Zuhura Ame alisema hali za baadhi ya wananchi waliopata maafa hayo sio nzuri hivyo wanahitaji msaada wa dharura.

Alisema kwamba licha ya viongozi wa majimbo hasa Wabunge, wawakilishi na madini baadhi yao tayari wameanza kutoa msaada na wengine ndio wanajipanga kufika kwa ajiri ya kuwafariji wananchi lakini bado panahitajika nguvu za pamoja baina ya wananchi, vyama vya kisiasa na serikali ili kuinusuru nchi kuingia katika maafa makubwa.

Naye Mkaanzi wa Mwanakwerekwe, Mwajuma Salum aliomba serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara inayohusika na masuala ya Miundombinu kutoa kipaumbele cha kujenga madaraja makubwa na yenye viwango katika maeneo mbali mbali nchini ili kuepusha hasara inayotokana na mvua hizo kila mwaka.

“ Tumesikia juzi tu serikali yetu imetangaza bajeti ya mwaka inayofikia Trioni moja, hivyo tunaomba kama inawezekana baadhi ya fedha zitumike katika uimarishaji wa miundombinu yetu kwani wengi tunateseka kwa sasa, mfano pale Mwanakwerekwe Gari za Shamba kuja mjini ni tabu kwani pale katika Bwawa la maji hakupitiki.”, alisema Mwajuma.

Alisema licha ya serikali kufanya ziara katika maeneo hayo bado baadhi ya wananchi hawana makaazi ya kuishi hivyo wanaiomba serikali iwapatie misaada ya dharura ili nao wapate huduma muhimu kwa kipindi hichi kigumu.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” aliwaagiza viongozi wa Serikali za Mitaa Zanzibar kuacha tabia ya kuruhusu uuzaji wa viwanja na ujenzi katika maeneo hatarishi hasa mabondeni na sehemu zinazotwaama maji ili kuepuka athari za mafuriko zinazoweza kusababisha vifo na uharibifu wa mali.

Maelekezo hayo aliyatoa katika Mtaa wa Tomondo Ziwa maboga na maeneo mengine wakati katika ziara yake ya kuwafariji wananchi waliopata athari za mafuriko katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Alisema wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kujilinda dhidi ya maisha yao kwa kuchukua tahadhari ya kutoishi katika maeneo wanayojua kuwa ni hatari juu ya afya na maisha yao.

Aliahidi kwamba CCM kwa kushirikiana na serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kuwasaidia wananchi waliopata athari hizo kwa Unguja na Pemba.

“ Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi natoa pole sana kwa wananchi wetu wa Zanzibar kwa Unguja na Pemba walioathiriwa na mvua hizi zinazoendelea kunyesha hivi sasa, kwa upande wa CCM tutaendelea kuwa nanyi kwa kutoa msaada wa Ari na Mali ili kuhakikisha mnarudi katika hali yenu ya kawaida.

Pia nakuombeni wananchi ifikie wakati na sisi tuisaidie serikali yetu kwa kuepuka kuishi ama kununua sehemu ambazo tunajua kwamba hazifai kuishi binadamu wakati mvua zinapoanza kunyesha.”, alisema Dkt. Mabodi na kuongeza kwamba CCM itaendelea kuwa karibu zaidi na wananchi kwa lengo la kuwapunguzia changamoto hizo.

Dkt. Mabodi aliishauri serikali kuchukua hatua za haraka za kurekebisha miundo mbinu ya barabara, maji na umeme kwa baadhi ya maeneo yaliyokubwa na mafuriko hayo ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu za kijamii.

Aidha alitoa wito kwa wananchi ambao kwa sasa makaazi yao bado yapo salama kujitolea kwa kuwasaidia wenzao waliopata maafa huku Chama kwa kushirikiana na serikali wakitafuta njia mbadala za kusaidia katika maeneo hayo.

Sambamba na hayo aliitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutembelea katika maeneo yaliyopata athari hizo kwa kugawa dawa za kutibu maji ya kunywa sambamba na kutibu visima ambavyo maji yake hayo salama kwa lengo la kuwanuru wananchi wasipate maradhi ya miripuka kwa kipindi hichi cha kuelekea katika Mwezi wa Ramadhani.

Alisema sululisho la kumaliza tatizo la maafa hayo yanayotokea kila mwaka ni lazima wananchi waache kujenga katika mitaro ya kusafirisha maji, hali inayosababisha maji hayo kukosa njia za kupita na kuwaathiri wananchi wengine wasiokuwa na hatia.

Naibu Katibu Mkuu huyo, Dkt. Mabodi katika ziara hiyo amefuatana na uongozi wa Mkoa wa Magharibi na Wilaya ya Dimani akiongozwa na Mwenyeji wake Mwenyekiti wa Mkoa huo , Yussuf Mohamed Yussuf na alitembelea maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi mengi yakiwa katika Wilaya ya Maghatibi ‘’B” ambayo ni Tomondo, Mwanakwerekwe Sokoni, Mwanakwerekwe Meli nne, Fuoni Migombani na Fuoni Chunga.

No comments: