Tuesday, May 16, 2017

CCM ZANZIBAR YAAHIDI KUENZI USHIRIKIANO NA CHAMA CHA CPC CHA CHINA

 Balozi mdogo wa China Zanzibar Bw. Xie Xiaowu pamoja na  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo la CCM Kisiwandui Zanzibar. 

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Juma Abdalla Saadala “Mabodi” amesema Chama cha mapinduzi (CCM) kitaendelea kuenzi kwa vitendo ushirikiano uliodumu zaidi ya karne moja baina ya chama hicho na Chama Cha Ukombozi cha China (CPC).
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Balozi Mdogo China Zanzibar Bw. Xie Xiaowu uliotembelea Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar.
Amesema ushirikiano uliopo baina ya vyama na serikali za nchi hizo zimeimarika na kuzaa matunda yanayowanufaisha wananchi wa pande zote  mbili katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Dkt. Mabodi alieleza kwamba njia pekee ya kulinda hazina hiyo ni kuwarithisha Vijana  Elimu na ujuzi zitakazowasaidia kupata uwezo wa kitaaluma  wa kulinda urithi huo dhidi ya maadui na wapinga maendeleo wa nchi hizo.
 “ Ushirikiano baina ya CPC na CCM ni ya muda mrefu hivyo sisi vizazi vya sasa ni lazima tujivunie huku tukiyalinda ili tuendele kunufaika na fursa za nchi hizo.
Kwa upande wake Balozi Mdogo wa China Bw. XIE XIAOWU ameahidi kwamba China itatoa ushirikiano wa Ari na Mali ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa nchi yenye nguvu kiuchumi na kijamii.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano baina ya vyama hivyo na serikali zake ili viweze kutekeleza kwa ufanisi mikakati ya kimaendeleo iliyoachwa na Viongozi Wakuu wa taasisi hizo toka enzi za kusaka uhuru wa nchini hizo.
Sambamba na hayo Balozi huyo Bw. Xie Xiaowu alisifu juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayotokana na CCM kuwa zinaongeza ushawishi na nia ya China kuendelea kusaidia sekta mbali mbali nchini ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Pamoja na Hayo alimpongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mabodi kuwa ni kiongozi mchapakazi kutokana na kuwa karibu na taasisi za kimataifa pamoja na wananchi kwa ujumla licha ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwa muda mfupi.
“  China inathamini juhudi mikakati mbali mbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi kwa lengo la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, hivyo na sisi  bado tuna nia na mikakati ya muda mrefu ya kuwaunga mkono kupitia  sekta za Afya, Elimu, Uvuvi na Miundombinu”, alifafanua Balozi huyo wa China.
Baada ya ziara hiyo Ujumbe wa China ulitembelea sehemu mbali mbali za makumbusho zikiwemo sehemu aliyouliwa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mwenyekiti wa balaza la mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Karume kisiwa ndui mjini     zanzbar.

No comments: