Picha ya juu na chini ,Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd akizungumza na Wadau wa Maendeleo na viongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF ofisini kwake mjini Unguja.
Picha ya pamoja
Balozi Seif Ali Idd akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga baada ya kupata maelezo ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo kisiwani Zanzibar,anayewaangalia ni Msimamizi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia ,Bwana Muderis Mohamed.
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Kizimbani,Unguja ambaye anatoka kwenye Kaya ya Mlengwa Wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini akikokotoa hesabu, anayemwangalia ni Msimamizi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Bwana Muderis Mohamed.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga(aliyesimama)akizungumza na baadhi ya wananfunzi wanaotoka katika Kaya za Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika shule ya msingi Kizimbani kisiwani Zanzibar.
Msimamizi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia akiwa katika picha na baadhi ya kununua kikapu kilichotengenezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini huko Kizimbani, kisiwani Zanzibar. Nyuma yake ni bidhaa zilizotengenezwa na walengwa hao kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
NA Estom Sanga- Zanzibar
Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Balozi Seif Ali Iddi amesema mchango unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika kuhamasisha wananchi kupambana na umasikini unapaswa kuungwa mkono kwani unakwenda sambamba na dhamira ya serikali zote mbili za kuwaondolea wananchi kero ya umasikini.
Balozi Iddi ametoa kauli hiyo alipokutana na baadhi ya wadau wa Maendeleo na Maafisa wa TASAF ofisini kwake mjini Unguja baada ya viongozi na wadau hao wa maendeleo kuhitimisha ziara ya kuwatembelea Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini kisiwani humo.
Amesema mafanikio makubwa yanayojitokeza katika nyanja za elimu, afya na ongezeko la shughuli za kiuchumi miongoni mwa walengwa wa Mpango huo ni ushahidi tosha kuwa wananchi hususani wale ambao wamekuwa wakikabiliwa na umasikini , wanahitaji kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa shughuli za Mpango huo ambao umekuja kwa wakati hasa kutokana na ukubwa wa tatizo la umasikini nchini.
Balozi Iddi amesema kwa kutambua hilo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono utekelezaji wa shughuli za TASAF kisiwani humo na kuwataka wananchi hususani wale walioko kwenye Mpango wa kunusuru kaya masikini kutumia fursa hiyo vizuri ili hatimaye waweze kuboresha maisha yao.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga amesema hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuweka msukumo wa kutosha katika utekelezaji wa Mpango huo zimeendelea kuzaa matunda ambapo katika maeneo mengi nchini kote walengwa wameonyesha kuanza kubadilika kwa kuboresha maisha hususani katika nyanja za makazi, elimu, afya na kuunda vikundi vya kuweka akiba na vya uzalishaji mali.
Kwa Upande wake Msimamizi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia,Bwana Muderis Mohamed, amesema wadau wa maendeleo wameonyesha kuridhishwa na matokeo mazuri yaliyoanza kuonekana kwa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya masikini jambo linaloendelea kuwavutia wadau wengi kujitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya Mpango huo.
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF inaendesha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini nchini kote ambapo takribani kaya MILIONI MOJA NA LAKI MOJA zinazokadiriwa kuwa na wakazi takribani walengwa milioni SITA zinanufaika na mpango huo.
No comments:
Post a Comment