|
|
Dar
es Salaam, TANZANIA. Taasisi na Asasi Zisizokuwa za Kiserikali za Tanzania
(NGOs) taasisi za serikali zinazoshughulikia uwajibikaji na wadau wengine
kadhaa walikutana hivi leo ili kufanya
tathmini ya hatua zilizopigwa na mafunzo yaliyopatikana wakati wa uhai wa mradi
wa Pamoja Twajenga unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia
Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID). Toka mwaka 2013,
watendaji wa mradi wa Pamoja Twajenga wamekuwa
wakifanya kazi bega kwa bega na asasi za kiraia na taasisi za serikali ya
Tanzania zinazoshughulikia masuala ya uwajibikaji ili kuimarisha mahusiano kati
ya asasi za kiraia na serikali. Mradi huu ulitoa mafunzo na msaada kwa jumla ya
asasi zisizo za Kiserikali 16 na taasisi tatu za serikali zinazojihusisha na
uwajibikaji katika mikoa ya Mtwara, Iringa, Dodoma, Morogoro na Zanzibar kwa lengo la kukuza uwazi na
uwajibikaji wa serikali kwa raia wa Tanzania.
Kutokana
na msaada huu, hivi sasa asasi za kiraia na taasisi za uwajibikaji
zilizoshiriki zina uwezo zaidi wa kushiriki katika mijadala kuhusu masuala
mahsusi yanayozigusa jamii (issue-based dialogue).
Raia katika mikoa lengwa
ya mradi – ikiwa ni ni pamoja na vijana, wanawake na makundi mengine ya watu
wanaowekwa pembezoni wana uwezo zaidi wa kujadiliana na serikali zao kuhusu
kero zao, jambo ambalo limeongeza uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa
rasilimali za umma na katika ufanyaji maamuzi. Asasi za kiraia zilizosaidiwa na mradi wa Pamoja Twajenga zinafanya kazi katika masuala
yanayohusiana moja kwa moja na mahitaji ya msingi ya raia ikiwa ni pamoja na
huduma za afya, elimu, usalama wa chakula na usimamizi wa rasilimali.
Mathalan, wanakijiji katika
kijiji cha Kibaigwa, mkoani Dodoma walikuwa wakilazimika kwenda umbali wa
kilomita 45 ili kupata kituo cha afya chenye huduma ya wodi ya wazazi. Asasi ya
Kiraia iliyofadhiliwa na mradi huu itwayo TACOSODE,iliwasaidia wanakijiji hao kujadiliana
na uongozi wa kijiji chao kuhusu haja ya kumalizia wodi mpya ya akinamama.
Mjadala huo uliifanya kamati ya kijiji kuwasilisha katika serikali ya wilaya
ombi la fedha kwa ajili ya kazi hiyo. Ujenzi wa wodi hiyo ulikamilika mwezi
Oktoba 2015 na hivi sasa inahudumia jamii.
Asasi
nyingine iliyosaidiwa na mradi wa Pamoja
Twajenga ni Chama cha Wanasheria watetezi wa Mazingira (LEAT) ambayo ilitoa
mafunzo ya usimamizi wa maliasili na uwajibikaji kwa jamii (social
accountability) kwa kijiji cha Kiwere mkoani Iringa. Mafunzo haya yaliwawezesha
wanakijiji kuchukua hatua ya kutaifisha mbao ambazo zilikuwa zimevunywa isivyo
halali katika ardhi yao.
Kupitia
misaada mbali mbali kwa asasi za Kiraia za Kitanzania na taasisi za serikali za
uwajibikaji mradi wa Pamoja Twajenga umesaidia kuimarisha mfumo wa majadiliano na
ushiriki ambapo asasi zinaweza kupata matokeo makubwa na endelevu zikiwa kama
asasi za ushawishi na utetezi katika sekta zao mahsusi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa leo, Naibu
Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania David Thompson alisisitiza, “mradi huu
umejielekeza katika azma moja kuu iliyo rahisi kueleweka: kwamba mstakabali wa
Tanzania unategemea ushiriki huru na imara wa raia kutoka katika nyanja zote za
maisha. Nyote mliokusanyika hapa hivi leo, iwe mnawakilisha asasi za kiraia au
Serikali ya Tanzania mmekuwa na mchango mkubwa katika kufikia azima hii.
Asanteni kwa ubia wenu. Tanzania imechukua hatua muhimu katika kuinua uwazi, kuimarisha
utoaji huduma za jamii, kuhakikisha kuwepo kwa nafasi ya kidemokrasia na
kuwasaidia raia kuchagiza mabadiliko.”
No comments:
Post a Comment