Tuesday, April 18, 2017

UKARABATI WA KIVUKO CHA MV PANGANI WAFIKIA HATUA ZA MWISHO

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu ametembelea na kukagua kivuko cha MV PANGANI II ambacho kinafanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza katika eneo la Pangani. Awali kivuko hicho kilikuwa kikitoa huduma kati ya Pangani na Bweni kabla ya ujio wa kivuko kipya cha MV TANGA.

Dkt. Mgwatu amejionea kazi zilizokamilika zikiwa ni pamoja na matengenezo ya milango mipya ya kupandia abiria na magari na sasa kiko katika hatua za mwisho za ukarabati wake. Aidha, Dkt. Mgwatu aliweza pia kusafiri kutoka upande wa Pangani hadi Bweni kwa kutumia boti mpya ya MV BWENI iliyojengwa hivi karibuni kwa ajili ya matumizi ya dharura katika eneo hilo.

Akiwa katika ukaguzi huo, Dkt. Mgwatu aliambatana na Meneja wa TEMESA Mkoa wa Tanga Mhandisi Margaret Gina, Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bw. Abdulrahman Amier pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa TEMESA mkoani Tanga.

Vile vile, Dkt. Mgwatu alipata wasaa wa kuzungumza na wafanyakazi wa Kivuko cha MV TANGA ambacho kinaendelea kutoa huduma katika eneo hilo na kuwaasa kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuhakikisha wanaongeza mapato. Aliwaomba wafanyakazi hao kuitunza boti ya MV BWENI ambayo itatoa huduma za dharura hasa wakati wa usiku kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na pia kutoa usafiri mbadala pale changamoto mbalimbali zitakapojitokeza.

Nae Mhandisi Gina alimueleza Dkt. Mgwatu kero mbalimbali wanazokumbana nazo kivukoni hapo ikiwemo kukosekana kwa vyumba vya ofisi kwa ajili ya wafanyakazi na kumuomba awasaidie kupata eneo kwa ajili ya kujenga ofisi. Dkt. Mgwatu alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu katikati akishuka kutoka kwenye chumba cha kuongozea kivuko cha MV Pangani kilichoko Pangani Tanga alipokuwa akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho. Nyuma yake ni Mkuu wa Kivuko Bw. Abdulrahman Ameir.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu wa pili kulia akikagua Kivuko cha MV Pangani kilichoko Pangani Tanga kinachofanyiwa ukarabati na kampuni ya MS Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza wakati wa ziara yake mkoani Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dk. Mussa Mgwatu aliyesimama katikati akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Kivuko cha MV Tanga kinachoendelea kutoa huduma kati ya Pangani na Bweni mkoani Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu akifurahia jambo na mmoja wa wafanyakazi wa boti ya MV Bweni mara baada ya kumaliza kikao na wafanyakazi wa TEMESA kituo cha Pangani mkoani Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu wa tatu kushoto akiwa ndani ya boti ya MV Bweni mara baada ya kumaliza kukagua kivuko cha MV Pangani kilichoko Pangani mkoani Tanga. Boti hiyo itatoa huduma za dharura ikiwemo kusafirisha wagonjwa nyakati za usiku.
Muonekano wa Kivuko cha MV Pangani kilichoko Pangani mkoani Tanga kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza.

No comments: