Thursday, April 20, 2017

TUNISIA YARIDHIA TAMKO KURUHUSU WATU BINAFSI KUPELEKA KESI ZAO MOJA KWA MOJA KWENYE MAHAKAMA YA AFRIKA IILIYO JIJINI ARUSHA


Tunisia imesema Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) ni lazima itangazwe kwa nguvu zote ili kuwawezesha wananchi barani Afrika kufahamu uwepo wake,malengo ya kuanzishwa kwake pamoja na shughuli zake.
Akipokea ujumbe wa Mahakama hiyo katika Ikulu ya Tunisia,Rais wa Nchi Hiyo ,Mh.Beji Caid Essebsi alipongeza uanzishwaji wa Mahakama hiyo na kuongeza  kuwa inahakikisha ulinzi wa Haki za Binadamu Barani Afrika.    
 “Kwa njia hii,Haki za Binadamu Barani Afrika zitalindwa na kuhakikisha maendeleo endelevu ya demokrasia kwa wananchi” Aliuambia ujumbe huo uliohusisha majaji watatu akiwemo Rais wa AfCHPR,Jaji Sylvain Ore’.
Kwa upande wake Rais wa AfCHPR, Jaji Ore’ aliishukuru serikali ya Tunisia kwa kukubali kuupokea ujumbe wake na kukutana na Viongozi na Maafisa mbalimbali wa nchi hiyo na pia kuendesha semina kwa wadau mbalimbali nchini humo kwa lengo la kuitangaza Mahakama.
Wakati wa ziara hiyo,Tunisia ilitia saini tamko la kuruhusu watu binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO’s) katika nchi hiyo kupeleka kesi zao moja kwa moja katika Mahakama hiyo yenye Makao yake makuu Jijini Arusha.
Hatua hiyo ya Tunisia ambayo ni utekelezaji wa kifungu cha 34(6),Inalifanya Taifa hilo kuwa Nchi ya nane Barani Afrika kukubali makundi hayo kupeleka kesi katika Mamlaka za Mahakama hiyo.
Nchi nyingine ambazo ni Wanachama wa umoja wa Afrika zilizotoa tamko kukubali Watu binafsi na NGO’s kutoka katika Nchi zao kupeleka kesi katika AfCHPR ni pamoja na:Benin,Burkina Faso,Côte d’Ivoire,Ghana,Malawi,Mali na Tanzania.
Utiwaji saini wa tamko hilo ulifanywa na Waziri wa mashauri ya kigeni wa Tunisia,Mh.Khemaies Jhinaoui kwa niaba ya Serikali ya Nchi yake.
Rwanda ambayo hapo awali ilitia saini kukubali tamko hilo sasa imejitoa ingawa Mkutano wa Kilele wa Viongozi wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa,Ethiopia mapema mwaka huu uliitaka nchi hiyo kutafakari juu ya uamuzi wake huo.
Kwa upande wake Misri ambayo haijaridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa shughuli za Mahakama hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na kuahidi kuwa itaridhia itifaki husika.
Mahakama hiyo ilifanya ziara ya kikazi Nchini Tunisia na Misri kuanzia April 9 hadi 14 Mwaka huu kwa lengo la kukuza uelewa wa wadau mbalimbali juu ya uwepo ya Mahakama,Malengo yake na shughuli zake.
Tangu mwaka 2010,AfCHPR imefanikiwa kuendesha ziara 27 za kuelimisha katika Maeneo mbalimbali Barani Afrika na kuendesha Semina na Mikutano ili kukuza uelewa wa Masuala kuhusu ulinzi wa Haki za Binadamu Barani humo na kuhamasisha Nchi wanachama wa AU kuridhia mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo na kutoa tamko la kuruhusu watu binafsi na NGO’s kupeleka kesi zao Mahakamani hapo.
AfCHPR ilianzishwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika(AU) kwa mujibu wa kifungu namba 1 cha itifaki ya Mkataba ya Mahakama hiyo na ilianza shughuli zake rasmi Novemba,2006 kwa lengo la kuimarisha Haki za Binadamu na Watu Barani Afrika.

No comments: