Saturday, April 1, 2017

SOPHIA MJEMA KIPANDA MTI KILELE CHA SIKU YA UPANDAJI ILALA LEO

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema akipanda mti wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Upandaji Miti, kilichofanywa na Wilaya ya Ilala katika shule ya Msingi, Yangeyange, Kata ya Msongola wilayani humo mkoani Dar es Salaam. Wapili kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo ya Ilala Edward Mpogolo na Kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando

Msongola, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amewataka watendaji wa Manispaa kuhakikisha wanazuia shughuli za kibinadamu ikiwemo ujenzi na kilimo katika maeneo oevu ili kulinda mazingira.

Amewasisitizia wananchi umuhimu wa kupanda miti mingi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuzuia magonjwa mbalimbali ambayo yamekuwa yakisababishwa na hali ya hewa.Mjema amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji miti duniani, ambayo wilaya ya Ilala iliyafanya shule ya msingi Yangeyange katika Kata ya Msongola wilayani humo.


Alisema mbali na kutunza mazingira na kuleta mvua, miti imekuwa ikitumika kama dawa na jambo la muhimu ni kuwa miti hiyo inafyonza mionzi inayotoka katika jua. “Miti hii inafyonza mionzi mikali inayotoka kwenye jua, ile mionzi badala ya kuja kutugonga moja kwa moja kwenye ngozi zetu inapita kwanza kwenye miti, miti hii inatukinga na maradhi hasa ya kansa. Lakini sasa mkiangalia maradhi ya kansa yanazidi hasa ya ngozi, miti tunakata sana, tupande na tutunze miti,” alisema mjema.

Akizungumzia kuhusu wananchi wanaojenga katika maeneo oevu na mabondeni, aliwataka watendaji na wenyeviti wa maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo kuhakikisha wanazuia mapema ujenzi huo badala ya kusubiri mtu anamaliza ujenzi na ndipo waende kumhoji.

Alitaka maeneo ya mabonde yote kupandwa kwa miti mbalimbali na kuwekewa mipaka hatua ambayo itasaidia kuhifadhi vyanzo vya maji, kuepusha mafuriko kwa wananchi lakini pia uvamii wa maeneo na kuingiza serikali katika migogoro.“Tusingoje mpaka mtu ameshafikisha nyumba yake juu, ndio unaenda kumuuliza nani kakwambia ujenge, ulikuwa wapi mtu anaanza kuchimba msingi hadi anamaliza, hilo ni agizo,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya watu wamkuwa na tabia ya kupanda miti ya nje ya nchi ambayo imekuwa ikihatarisha miti ya asili kama mpingo, mivule na mining ambayo kama ikipandwa itasaidia kutunza kurudisha uoto wa asili na kutunza kumbukumbuku kwa kizazi kijacho.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya amezikumbusha Halmashauri zote za Dar es Salaam, kuhakikisha zinapanda upya miti iliyokufa ambayo ilipandwa katika barabara kuu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Mti wangu”.Maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu yana kauli mbiu ya “Panda miti, tunza misitu, upate nishati”.

Mjema alisema kwa kupanda miti tuafikisha malengo tuliyojiwekea ya kupanda miti milioni nne ifikapo 2019.Kwa mujibu wa takwimu, takribani hekta 372, 8721 hupotea kila mwaka kwa ajili ya nishati na pia hubadilishwa kwa shughuli za kilimo cha kuhahama na ujenzi.

Aidha, matumizi ya nishati na mbao kwa mwaka inakadiriwa mita za ujazo milioni 72, wakati uwezo wa misitu ya hapa nchini ni mita za ujazo milioni 43 ambazo ni chini ya kiwango kinachohitajika. Kwa kuzingatia uvunaji endelevu nchi yetu ina upungufu wa mita za ujazo milioni 19 .

“Twakwimu zinaonesha Mkoa wetu tunatumia nusu ya matumizi ya nchi nzima, kiwango hiki ni kikubwa hivyo hatuna budi tupande miti ili tukabiliane na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Mjema

No comments: