Shirika la Anga la Etihad limetangaza uteuzi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Idara yake tanzu ya Airline Equity partners, Bwana Robin Kamark ambaye atashughulikia kuongoza na kuendeleza mikakati ya uwekezaji inayojumuisha wabia wa Shirika hilo kama vile; Airberlin, Alitalia, Jet Airways, Air Serbia, Air Seychelles, Etihad Regional na Virgin Australia.
Mtendaji huyo mkuu atakuwa chini ya Rais wa Shirika hilo na Mkurugenzi Mkuu. Kamark anachukua nafasi ya Bruno Matheu ambaye alishika wadhifa huo tangu Mei 2016 ambaye imeelezwa kwamba anaachia ngazi kutokana na sababu zake binafsi.
Kamark amefanya kazi katika sekta ya anga kwa takriban miaka 17, huku akifanikiwa kufikia malengo ya mikakati yake ya kibiashara na masuala ya utawala katika Shirika la SAS ambako pia alikuwa akitekeleza majukumu yake kama Ofisa Mkuu wa Biashara.
Kwa miaka mitano yake ya mwishoni amefanya kazi kama Makamu wa Rais na Ofisa Mkuu wa Biashara katika kitengo cha bidhaa za ASA zinazoongoza kwa huduma za kifedha na biashara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Anga la Etihad, Mhe. Mohamed Mubarak Fadhel Al Mazrouei amesema kwamba “Shirika hili linaendelea kuwekeza duniani katika kiwango chenye ubora wa juu, ikiwamo kujenga timu nzuri itakayoongoza biashara na kuipelekea katika hatua kubwa zaidi za maendeleo.”
Alisema, “Robin ni kiongozi anayeheshimika katika sekta ya anga duniani pia ana uzoefu mkubwa kutoka Shirika la SAS. Amefanya kazi kubwa ya kuboresha shirika hilo la ndege. Hivi karibuni amepanua wigo wa taaluma yake katika masuala ya huduma za kifedha.”
Aliongeza kuwa, “Ushirikiano na kampuni yetu utaendelea kuwa alama muhimu katika biashara na Robin ataongoza mipango hiyo kwa kuweka mikakati na kuendeleza dhamira yetu.”
“Tunapenda kumshukuru Bruno kwa juhudi zake kubwa alizoonyesha kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kutokana na kufanikiwa kujenga na kuhimarisha ushirikiano wetu katika kitengo cha Airline Equity partners,” alisema kiongozi huyo.
Kamark ataongoza mikakati ya maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika biashara, mapato na kuboresha bei baina ya Shirika la Ndege la Etihad na wabia wake ulimwenguni. Pia atasimamia mikakati ya kiutawala kwa wabia wa mashirika ya ndege ambayo Shirika la Etihad linashirikiana nayo.
Kamark amepata elimu ya shahada ya kwanza na uzamili katika masula ya uongozi wa biashara, huku akifuzu kwenye Shule ya Utawala ya Norwegian.Alianza kazi ya uhasibu katika sekta ya viwanda vya uzalishaji bidhaa, pia alitumikia jeshi kabla ya kujiunga na SAS mwaka 1995.Kamark ataanza majukumu yake rasmi Oktoba mwaka huu.
Akishukuru uteuzi huo Kamark alisema, “Ninaishukuru Bodi ya Shirika la Anga la Etihad kwa ujasiri wao wa kuniteua. Haya ni majukumu makubwa, kunipa nafasi hii muhimu kuendeleza na kuboresha mikakati muhimu ya Shirika.”
Ofisa Mikakati na Mipango wa Shirika hilo, Kevin Knight ataungana na Bruno Mathew katika kuendeleza Idara ya Airline Equity Partners.
Kamark anakuwa miongoni mwa watendaji wa juu katika Shirika la Anga la Etihad akiungana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Etihad (Peter Baungartner), Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhandisi cha Shirika la Ndege Etihad (Jeff Wilkinson), Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Uwanja wa Ndege (Chris Youlten).
Uongozi wa Shirika la Hala linalohusika na masula ya Masoko na Huduma za Hadhi ya juu, watatangaza mkurugenzi wake wa kudumu mwishoni mwa mwaka huu.
Bodi ya Shirika la EAG kwa sasa linaendelea na mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu wake mpya ambaye atachukua nafasi ya Rais na Mkurugenzi wa sasa, James Hogan ambaye awali ilitangazwa ataachia ngazi baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment