Monday, April 3, 2017

SADC YALIPONGEZA BARAZA LA USALAMA LA UN KWA KUONGEZA MUDA KWA MISHENI YA ULINZI DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York, Marekani na kupitisha Azimio la kuongeza muda kwa vikosi vya usalama vilivyopo DRC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy. 
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Mahiga (hayupo pichani). 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb). akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani. 
 ============================================= 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amelipongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kwa kuridhia na kupitisha azimio namba 2348 (2017) la kuongeza muda kwa Misheni ya Ulinzi wa Amani chini ya MONUSCO iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi tarehe 31 Machi, 2018.

Mhe. Mahiga ametoa pongezi hizo wakati akihutubia Baraza hilo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani hivi karibuni.

Mhe. Mahiga ambaye aliwakilisha nchi 15 za SADC alisema kuwa anaupongeza Umoja wa Mataifa kwa ujumla chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Bw. Antonio Guterres kwa kufikia uamuzi wa kuongeza muda kwa MONUSCO na jitihada nyingine nyingi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili DRC kwa muda mrefu ikiwemo ukosefu wa amani na usalama.

Mhe. Mahiga alisema kuwa, kupitishwa kwa azimio hilo kunatoa matumaini mapya kwa wananchi wa DRC na dunia kwa ujumla kwamba Umoja wa Mataifa una nia ya dhati kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.

Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kuuomba Umoja wa Mataifa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Kikosi Maalum cha Force Brigade Intervention-FIB kilichoundwa na SADC ambacho kinashirikiana na MONUSCO katika ulinzi wa amani nchini DRC. 

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa FIB kimeonesha uwezo mkubwa kwa kufanya operesheni ngumu za kukabiliana na vikundi vya waasi na kuvidhibiti, hali iliyopelekea MONUSCO kuaminika zaidi. FIB ina mchango wa vikosi vya ulinzi wa amani kutoka nchi tatu za SADC ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

“Kuanzishwa kwa FIB miaka minne iliyopita ulikuwa ni uamuzi wa pekee kwa Baraza la Usalama na SADC katika masuala ya ulinzi wa amani hususan kwenye maeneo yenye changamoto kubwa za usalama na amani. Hivyo naamini pamoja na kwamba FIB ni Chombo cha muda bado kinahitaji kutambuliwa na kupongezwa” alisema Waziri Mahiga.

Kuhusu changamoto mbalimbali ambazo MONUSCO inakabiliana nazo ikiwemo matishio mapya ya usalama katika maeneo ya Kivu, mbinu mpya za mashambulizi za waasi, ukatili kwa raia na ukiukwaji wa haki za binadamu Waziri Mahiga alisema masuala haya yanailazimu pia MONUSCO kubadilisha mbinu za operesheni ikiwemo kuongezewa vifaa na bajeti ili kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto hizo. 

Pia aliliomba Baraza la Usalama, SADC, Umoja wa Afrika, ICGLR na Nchi zinazoongea Kifaransa kushirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto zinazoikabili DRC kwa sasa.

Vile vile, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya SADC kuiomba na kuialika Jumuiya za Kimataifa kuisaidia Tume ya Uchaguzi ya DRC ili iweze kuandikisha wapiga kura na kuandaa uchaguzi nchi nzima. Pia aliwaomba wanasiasa wa nchini DRC kukabiliana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo kwa sasa na kukwamisha utekelezaji wa Mkataba uliofikiwa mwezi Desemba 2016 chini ya Baraza la Maaskofu (SENCO) la DRC.

Mhe. Mahiga aliongeza kusema kuwa SADC itatuma Misheni Maalum ya Mawaziri nchini DRC katika kipindi cha majuma mawili kuanzia sasa kwa ajili ya kwenda kuzungumza na kushauriana na wadau mbalimbali wa masuala ya siasa nchini DRC ili kutafuta suluhu.”Sisi , nchi wanachama wa SADC hatupo tayari kuona Mkataba wa Desemba unakwama” alisisitiza Waziri Mahiga.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 03 Aprili, 2017.

No comments: