Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea miradi ya maendeleo kisiwani Pemba ukiwemo mradi wa barabara, umeme na Chuo cha Mafunzo ya Amali na kuitaka Kampuni ya ZECON inayojenga Chuo hicho kuhakikisha mradi wa ujenzi huo unakamilika kwa muda uliopangwa.
Akiwa katika eneo la
chuo hicho huko Daya Mtambwe mara baada ya kupata maelezo kutoka kwa Kampuni ya
Ujenzi pamoja na Mshauri Mwelekezi alisisitiza kuwa mradi huo ni wa Serikali na
Wizara ya Elimu ni wasimamizi tu, hivyo alieleza umuhimu wa kumalizika mapema
mradi huo kwa maslahi ya wananchi.
Alieleza kuwa changamoto
za kiufundi zilizojitokeza katika kutekeleza mradi huo hazina budi kupatiwa
ufumbuzi wa haraka ili utekelezaji wa mradi huo uweze kukamilika kama
ilivyopangwa.
Mara baada ya kukagua
mradi wa ujenzi wa Chuo cha Amali kilichopo Daya Mtambwe, Dk. Shein alipata
nafasi ya kuzungumza na wananchi pamoja na wanafunzi wa Skuli ya Msingi Daya
katika viwanja vya skuli hiyo na kusisitiza lengo la Serikali la kujenga chuo
hicho.
Dk. Shein alisema kuwa
ujenzi wa Chuo hicho utawasaidia wale wanafunzi waliokuwa hawakupata fursa ya
kuendelea na masomo ya juu na kuweza kupata mafunzo ya vitendo yakiwemo mafunzo
ya kiufundi.
Alisema kuwa uwamuzi wa
Serikali ni kujenga chuo hicho kama kilivyo chuo cha Amali cha Vitongoji kwa upande
wa Pemba na Mkokotoni Unguja na kusisitiza kuwa ujenzi huo utakwenda sambamba
na ujenzi wa chuo cha Amali huko Makunduchi.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa ujenzi wa Chuo hicho ni ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi mkuu
uliopita wakati akiwahutubia wananchi huko Kangagani, na kusisitiza utekelezaji
wa ahadi yake hiyo upo pale pale.
Alisema kuwa licha ya
ujenzi huo kusita kutokana na sababu za kiufundi kwa takriban miezi saba kwa
hivi sasa na kueleza kuwa si zaidi ya wiki tatu ujenzi huo utaendelea na
matarajio ni kumalizika hapo mwakani.
Mapema Dk. Shein alipata
fursa ya kukagua ukarabati wa barabara ya Chwale (Madenjani) hadi
Mzambarautakao wenye urefu wa kilomita 5 unaoendelea kwa kiwango cha lami ambao
unatarajiwa kumalizika baada ya wiki moja.
Mkuu wa Mradi kutoka
Kampuni ya MECCO, Crispin Prosper Mwombeki, alimueleza Dk. Shein kuwa ukarabati
huo baada ya miezi saba umefanywa kwa muda wa miezi mitatu ili kwenda na hali
halisi ya jiografia ya Pemba.
Pamoja na hayo, Mwombeki
alieleza changamoto zilizopo hasa katika suala zima la utaratibu wa upatikanaji
wa kifusi kwa ujenzi wa barabara huku akieleza haja ya kuweko na utaratibu wa
kudumu wa ukarabati wa barabara hizo ndani ya mwaka mmoja.
Wakati huo huo, Dk.
Shein alifika Ukunjwi kwa ajili ya kuangalia mradi wa umeme unaopelekwa katika
kisiwa cha Fundo.
No comments:
Post a Comment