Thursday, April 20, 2017

PROF. MUHONGO AZINDUA BODI YA REA

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akizungumza na Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini - REA (hawapo pichani), wakati alipokuwa akiizindua rasmi Bodi hiyo Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Aprili 19, 2017.

Na Veronica Simba – Dodoma
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, amezindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuiagiza kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.
Profesa Muhongo alizindua Bodi hiyo jana, Aprili 19, 2017 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Akizungumza na Wakurugenzi wa Bodi hiyo mpya, wakati wa hafla ya uzinduzi, Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi waliochaguliwa kutekeleza miradi ya umeme vijijini ili wanunue vitendea kazi ikiwemo nguzo, transfoma na nyaya za umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ya nchi.

“Wakandarasi ni lazima wanunue vifaa hivyo ndani ya nchi. Vikiisha hapa nchini, ndiyo waagize nje. Hatutavumilia kuona mkandarasi ananunua vitendea kazi nje ya nchi wakati hapa nchini vipo tele.”

Hata hivyo, Profesa Muhongo alisisitiza suala la ubora ambapo alifafanua kuwa, ni lazima vitendea kazi vinavyonunuliwa viwe katika ubora unaostahili. “Japokuwa tunataka vitu kutoka ndani ya nchi lakini ni lazima tuzingatie suala la ubora wake.”

Akiendelea kutoa maagizo kwa Bodi hiyo, Waziri Muhongo pia alielekeza kwamba, Kampuni zote za kigeni ambazo zimeshinda Tenda ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini awamu ya Tatu (REA III), ni lazima zifanye kazi na wakandarasi wadogo (sub-contractors) wa kitanzania.
“Ni lazima wakandarasi wadogo wote watoke Kampuni za Kitanzania. Inaweza kuwa Kampuni iko hapa nchini lakini siyo ya watanzania; hiyo hatuitaki. Mradi huu unalenga kuwawezesha watanzania hivyo ni lazima wapate fursa,” alisisitiza Waziri.

Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuhamasisha watanzania wenye sifa kujitokeza kwa wingi ili wafanye kazi na kampuni kubwa za wakandarasi kutoka nje, na baadaye waweze kujitegemea na kujenga uwezo wa kufanya kazi hizo wao wenyewe.

Aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha wanatatua changamoto ya baadhi ya vibarua kutokulipwa malipo yao baada ya kufanya kazi. Aliwataka kuweka usimamizi utakaowezesha kila mmoja kulipwa stahili zake kulingana na kazi aliyofanya.

Vilevile, Profesa Muhongo aliitaka Bodi kusimamia ubora wa kazi inayofanywa na wakandarasi husika kwani kutokana na uzoefu inaonesha kwamba, baadhi yao, kazi zao hazina ubora unaoridhisha.

Alisema, Bodi inawajibika kumfuatilia kila Mkandarasi kujiridhisha kuhusu uwezo wake, hata kama ameshapitishwa na taratibu za manunuzi. Alisema, endapo Bodi itakuwa na wasiwasi na uwezo wa Mkandarasi, ni lazima iweke hilo wazi kwani kazi isipofanyika ipasavyo, hawatakwepa lawama.

“Iteni kampuni moja baada ya nyingine mjiridhishe na utendaji wao. Muone eneo alilopewa, ukubwa wa eneo hilo na bajeti aliyopewa. Pia mumuulize kuhusu vitendea kazi alivyonavyo pamoja na wataalam alionao,” alisisitiza.

Aidha, Profesa Muhongo aliwataka wakurugenzi wa Bodi hiyo kujenga utaratibu wa kutembelea maeneo inakotekelezwa miradi mbalimbali ya umeme vijijini ili kujionea kwa macho maendeleo ya kazi inayofanyika.

Suala jingine muhimu ambalo Waziri aliwaelekeza wakurugenzi wa Bodi kulifanyia kazi, ni kupitia taarifa ya utekelezaji wa REA II ili pamoja na mambo mengine, waweze kujiridhisha na majina ya wakandarasi waliopitishwa kutekeleza REA III. Aliwataka kumkataa Mkandarasi ambaye watabaini amepewa Tenda kutekeleza REA III wakati alishindwa kazi REA II.

Pia, Waziri Muhongo aliitaka Bodi kuwafuatilia wakandarasi husika ili kuhakikisha wakati wanasambaza umeme vijijini katika awamu hii ya Tatu, wanatoa kipaumbele kwa maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na Taasisi za jamii kama vile shule, ofisi mbalimbali za uongozi, nyumba za kuabudu, sehemu za biashara na uzalishaji. “Watu wa mashambani wasiwe wanakuja wizarani kuomba umeme. Umeme upelekwe kwenye mashamba na hata kwenye Ranchi mbalimbali. Hatutaki kusikia mtu anarukwa,” alisisitiza.

Sambamba na maelekezo hayo yote, Profesa Muhongo pia aliitaka Bodi husika, katika kikao chake cha kwanza, ijadili na kupendekeza namna ya kuongeza asilimia ya watanzania wenye fursa ya kupata umeme, kutoka ile iliyopo sasa ambayo ni asilimia 49.5.

“Mje na mapendekezo mnataka tufike asilimia ngapi na kwa kutumia mbinu zipi.”

Awali, akizungumza na wakurugenzi wa Bodi mpya iliyoteuliwa, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, aliwataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija kwa Taifa.

Profesa Mdoe aliwataja wakurugenzi wa Bodi mpya ya REA walioteuliwa kuwa ni Dkt. Gideon Kaunda ambaye ni Mwenyekiti pamoja na wajumbe Mhandisi Innocent Luoga, Happiness Mhina, Stella Mandago, Scholastica Jullu, Amina Chinja, Theobald Sabi na Michael Nyagoga.

Alisema kuwa, Waziri Muhongo, amefanya uteuzi huo kutokana na Mamlaka aliyonayo, chini ya Kifungu Namba 5(1) (b) na Namba 8(3) cha Sheria ya Nishati Vijijini ya mwaka 2005, akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, kwa niaba ya Wakala huo, aliahidi kutoa ushirikiano stahiki kwa Bodi iliyoteuliwa ili kwa pamoja waweze kuleta matokeo chanya katika kuwapatia umeme wananchi walioko vijijini.

Uteuzi wa Bodi mpya ya REA ni wa miaka mitatu na umeanzia tarehe 1 Aprili, 2017.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (kulia), akiwasomea majukumu yao ya kazi, Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo, uliofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Aprili 19, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya REA, uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Baadhi ya Wakurugenzi/Wajumbe wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakizungumza mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), mara baada ya kuizindua rasmi hivi karibuni mjini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe na kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Gideon Kaunda. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwakabidhi vitendea kazi, baadhi ya wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na maofisa mbalimbali kutoka wizarani na REA, wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.

No comments: