Thursday, April 6, 2017

MUHIMBILI YAWAJENGEA UWEZO MADAKTARI WA HOSPITALI BINAFSI NA UMMA NCHINI KUFANYA UPASUAJI WA KISASA

 Daktari Bingwa aliyebobea katika Magonjwa ya Kinamama na Uzazi, Profesa Rafique Parkar akifanya upasuaji wa kutumia njia ya matudu madogo kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili leo. 
 Baadhi ya madaktari kutoka katika Hospitali za umma na binafsi nchini wakifuatilia mubashara upasuaji wa njia ya matundu madogo uliofanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imendelea kuwajengea uwezo madaktari wa ndani na nje ya hospitali kwa kufanya upasuaji wa njia ya matundu madogo (laparoscopic surgery).

Miongoni mwa madaktari walioshiriki kwenye upasuaji huo ni kutoka hospitali ya za jijini Dar es Salaam zikiwamo Kairuki, Tumaini, Regency na Agha kan. Madaktari wengine ni kutoka hospitali za umma zikiwamo Hospitali ya Temeke, Amana pamoja na hospitali za mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha, Morogoo na Dodoma.

Lengo ni kuwaongezea ujuzi madaktari hao ili waendelee kufanya upasuaji wa kutumia njia ya matundu madogo kwa wagonjwa mbalimbali.
Upasuaji huo unafanywa na madaktari wa muhimbili kwa kushirikiana na Daktari Bingwa aliyebobea katika magonjwa ya kinamama na uzazi, Profesa Rafique Parkar ambaye amekuwa akifanya upasuaji huo nchini Afrika Kusini, Kenya na nchi mbalimbali barani Afrika.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama na Uzazi, Vicenti Tarimo wa hospitali ya Muhimbili amesema wagonjwa wanne wamefanyiwa upasuaji na kwamba wengine watatu walikuwa wakiendelea kufanyiwa upasuaji huo leo.
“Leo wagonjwa wenye matatizo ya uzazi na wenye uvimbe wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia njia hii. Kesho wagonjwa wengine watano watafanyiwa upasuaji kwa kutumia njia hii,” amesema Dk Tarimo.

Dk. Tarimo amesema lengo ni kuwawezesha madaktari wa hapa nchini kutumia njia matundu madogo kufanya upasuaji badala ya kutumia njia ya kufungua tumbo ambayo mgonjwa anatumia muda mrefu kupona.

“Upasuaji wa njia ya matundu madogo una faida kubwa, kwanza mgonjwa anapona haraka tofauti na upasuaji wa kufungua tumbo. Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa njia hii ya kisasa wanaweza kuendelea na kazi kwani baada ya muda mfupi wanapona,” amesema Dk Tarimo.

Hospitali ya Muhimbili imekuwa ikifanya upasuajia wa njia ya matundu madogo na sasa inaongeza uwezo kwa madaktari mbalimbali nchini wakiwamo madaktari wa Muhimbili.

No comments: