Tarehe 24 Novemba 2016 Wizara
ilizindua Cheti kipya cha Chanjo za Kimataifa kijulikanacho kama Cheti cha Chanjo ya Homa ya Manjano ili
kuendana na maboresho ya kipengele cha 7 cha Kanuni za Afya za Kimataifa za
mwaka 2005.
Lakini pia, zoezi hili lililenga kukabiliana na kusambaa kwa vyeti
vya kugushi (feki) ambavyo watu wamekuwa
wakivipata bila kupata chanjo, hali ambayo ilitishia Afya ya Jamii dhidi ya
ugonjwa huo. Kwasababu hizo, Wizara iliona ni vema kufanya mabadiliko ya cheti
hicho, ambapo wenye vyeti vya zamani wanabadilishiwa na wale wanaopata chanjo wanapewa cheti kipya.
Wizara inapenda kutoa
taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo kama ifuatavyo. Kabla ya kuanza matumizi
ya vyeti vipya, wastani wa wasafiri 800 walikuwa wanapatiwa chanjo kwa mwezi
kupitia vituo vilivyoruhusiwa na Wizara. Baada ya kuzindua vyeti vipya na
kuongeza udhibiti wa vyeti feki idadi ya wanaopata chanjo imeongeza kutoka 800
hadi 2,445 kwa mwezi ikiwa ni ongezeko la mara 3 ya waliokuwa wanachanja hapo
awali. Ongezeko hili limesababishwa na wasafiri zaidi ya 1,644 kusalimisha
vyeti feki kwa mwezi na kuchanjwa na kupewa vyeti halali.
Kwa ujumla tangu matumizi ya
vyeti vipya vianze mwezi wa Agosti mwaka 2016 mpaka mwezi Machi 2017, jumla ya
wasafiri 19,557 wamepatiwa chanjo ambapo kati yao 13,157 wamesalimisha vyeti
feki na kupatiwa chanjo, hii ni sawa na asilimia 67.2. Halikadhalika, watu 11,644
wamebadilisha vyeti vyao halali vya zamani.
Kupata cheti bila kupata
chanjo ni kosa na kunahatarisha afya yako na Afya ya Jamii, kwani ukienda katika
nchi zenye hatari ya ugonjwa wa homa ya manjano, unaweza kuambukizwa kwasababu
huna kinga na hatimaye kuleta ugonjwa huo nchini. Vile vile zoezi hili
limebaini uwepo wa vituo vinavyotoa chanjo hii bila kuwa na kibali cha Wizara, hili
ni kosa na hivyo ni marafuku kituo chochote kutoa chanjo hiyo hadi hapo vituo
hivyo vitakapopata kibali. Aidha, kwa wale ambao wananunua au kutoa vyeti bila
kupata chanjo nao wanatenda kosa hivyo, waache mara moja kwani mkono wa sheria
utachukua mkondo wake.
Tarehe 16 Februari 2017 Wizara
ilikumbusha kubadili vyeti vya zamani katika muda uliopangwa yaani Januari 1
hadi Machi 31, 2017. Kutokana na tathmini tuliyoifanya imeonekana kuwa watu wengi
bado hawajabadili vyeti vya zamani na kutokana na umuhimu wa zoezi hilo kwa
afya ya jamii, tumeamua kuongeza muda wa mwezi mmoja ili watu wapate nafasi ya kubadili
vyeti vyao, hivyo zoezi hili litaendelea na litahitimishwa tarehe 30.04.2017. Wizara
inatoa wito kwa watu ambao bado wana vyeti vya zamani kufika katika vituo vya
kutolea huduma na kuvibadilisha. Baada ya muda huo kupita hakutakuwa na muda
mwingine wa nyongeza.
Wizara inawakumbusha tena
kuwa ugonjwa wa homa ya manjano haupo nchini ila kwa mujibu wa Shirika la Afya
Duniani, Tanzania ipo katika ukanda wa nchi zenye kiwango kidogo cha maambukizi
ya ugonjwa huo (low risk country). Hata hivyo, tupo katika hatari ya kuupata
ugonjwa huo kutokana na kuzungukwa na nchi zilizopo kwenye ukanda wa kiwango
cha juu cha hatari ya ugonjwa huo (High risk countries).
Hivyo ni jukumu la
kila mtu kuhakikisha tunajilinda dhidi ya ugonjwa huo kuingia nchini.
Ugonjwa huu husambazwa na
mbu jike aina ya Aedes aliye na
virusi vya ugonjwa huo. Mpaka sasa duniani hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huo na
mgonjwa hupatiwa matibabu ya kupunguza maumivu au kutibu dalili zinazojitokeza.
Njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huu ni kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Chanjo
hiyo huanza kufanya kazi kiufasaha siku kumi baada ya mtu kupata chanjo hiyo. Hivyo, nawasihi wanaosafiri kupata chanjo
hiyo angalau siku kumi au zaidi kabla ya kusafiri kwenda kwenye nchi zenye
maambukizi. Aidha,
kwa watu wasio na safari hawahitajiki kupata chanjo hiyo.
Vile vile, kwa wale ambao
hawastahili kupata chanjo kwa sababu za umri (miaka 60 na kuendelea),
wajawazito na watu wenye sababu za kiafya zilizothibitishwa na Daktari,
watapatiwa cheti maalaumu kijulikanacho kama
“International Vaccination Exemption certificate” pamoja na kupewa ushauri
wa hatua za kiafya za kuchukua dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Mwisho, Wizara inapenda kuwashukuru
wale wote walioitikia wito wa zoezi hili la kubadili vyeti kwani wamefanya
hivyo kwa manufaa yao na ya Taifa. Halikadhalika, wale ambao hawajabadili vyeti
vyao watumie muda huu wa nyongeza kufanya hivyo.
Imetolewa
na;
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini-Afya
21-04-2017.
No comments:
Post a Comment