Na
Lulu Mussa
Mwanga
- Kilimanjaro
Imebainika kuwa Ziwa Jipe
liko hatarini kutoweka endapo hatua za haraka hazitachukuliwa katika
kulinusuru. Hayo yamesemwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa
Mazingira Mh. January Makamba alipofanya ziara ya kukagua ziwa hilo ambalo
sehemu kubwa imezungukwa na magugu maji.
Waziri Makamba amesema
kuwa ziwa hilo ni rasilimali muhimu na hivyo ni lazima kuwe na mpango wa muda
mfupi na ule wa muda mrefu. Kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamiza wa
Mazingira (NEMC) ameazimia kutangaza kupita Tangazo la Serikali kuwa eneo hilo
ni eneo nyeti kimazingira."Tutatanga eneo hili kuwa eneo nyeti kimazingira
na tutaweka masharti ya matumizi katika eneo hili" Alisisitiza Makamba
Azimio hilo la kutangaza
kuwa eneo mahsusi ama nyeti kimazingira itasaidi katika kuandika maandiko
mbalimbali ya miradi na kupata fedha kutoka kwa wadau na washirika wa
maendeleo. Pia litawekwa chini ya uangalizi maalumu na kuweka masharti ya
matumizi bora ya eneo hilo. " Tutaweka masharti makali na magumu zaidi ili
watakao kiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria" Aliongezea Waziri
Makamba.
Aidha, Waziri Makamba
amesisitiza kuwa ni vema kunusuru ziwa hilo sasa maana ndani ya miongo 2-3
huenda ziwa hilo likatoweka. "Bila
hifadhi ya mazingira hakuna maisha, na ukiyaharibu mazingira hakuna msamaha
yatakuadhibu tu" Akiongea katika Mkutano wa hadhara kijijini Butu, Waziri
Makamba amesema kuwa shughuli zozote za maendeleo iwe uvuvi, kilimo, utalii,
mifugo kwa namna moja ama nyingine zinategema hifadhi endelevu ya mazingira.
Katika hatua za muda mrefu
Waziri Makamba amewataka wasimamizi wa Bonde la Pangani, Wizaya ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukutana mara moja kuandaa mpango na mtazamo wa
pamoja wa kunusuru Ziwa Jipe.
Akiwa njiani kuelekea
Nyumba ya Mungu Waziri Makamba alipitia katika Kiwanda cha Kifaru Quarries Co.
Ltd na kukuta kikiendelea na uzalishaji wa kokoto bila kuwa na cheti cha
Tathmini ya Athari kwa Mazingira. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) limeutaka uongozi wa Kiwanda hicho kusitisha uzalishaji mara
moja na kutakiwa kulipa faini kwa kukiuka Sheria ya Mazingira kifungu namba 81
na 196.
Waziri Makamba pia
amefanya ziara katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kufanya mkutano wa hadhara na
wakazi wa kijiji cha Kakongo ambao kwa pamoja wamelalamikia zuio la kufanya
shughuli za uvuvi katika bwawa hilo kutokana na kupungua kwa kina cha maji na
samaki katika bwawa hilo.
Bw. Charles John Waziri
Mkazi wa Kijiji cha Kagongo amesema kuwa kuna hujuma katika matumizi ya
rasilimali maji ambapo imebainika kuwa wakulima wanaotumia kilimo cha
umwagiliaji wamekua wakitumia maji kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu
katika bwawa.
Akijibu kero na malalamiko
ya wananchi hao Waziri Makamba ameagizia kufanyika kwa doria na kuainisha pampu
zote zinazovuta maji kutoka bwawani hapo "Naaagiza Mamlaka ya Wilaya ya
Mwanga, Serikali ya Mtaa na Mamlaka ya Bonde Pangani kufanya doria na kuhakiki
pampu zote kujua uhalali wake kama zimesajiliwa na kama zinavibali,
zitakazobainika kutokuwa na vibali zote zitaifishwe" Alisisitiza Waziri
Makamba.
Waziri Makamba yuko katika
ziara maalumu ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, changamoto na
kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu wa kukabiliana nazo. Mpaka sasa
Waziri Makamba ameshatembelea Mkoa wa Pwani, Tanga na Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment