Monday, March 20, 2017

ZANZIBAR YASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA MBALIMBALI BAINA YAKE NA SERIKALI NA MAJIMBO NCHINI INDIA

Zanzibar imeshauriwa kuchangamkia furSa mbali mbali za ushirikiano
zinapokezea baina yake na Serikali za Majimbo Nchini India katika
sekta za Kilimo, Biashara, Uwekezaji, Afya na huduma za Mawasiliano
kutokana na Taifa hilo liliopo Barani Asia kupiga hatua kubwa ya
Maendeleo kwenye Sekta hizo.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi
Mohamed Hija wakati akikiongoza Kikao cha matayarisho cha Ujumbe wa
Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi ambao tayari umeshawasili Nchini humo kwa Ziara ya Kiserikali
ya Wiki Moja.

Balozi Mohamed Hija alisema Zanzibar ina fursa pana ambazo bado
haijazitumia katika kujitanua kimawasiliano kwa kushirikiana na
Taasisi mbali mbali Duniani katika harakati zake za kujikwamua
kiuchumi na kuimarisha mipango yake ya Maendeleo hasa kwenye zile
Sekta zilizo nje ya Muungano.

Alisema India imebarikiwa kuwa na Taasisi na Makampuni mengi kwenye
Serikali za Majimbo ambazo zinaweza kusaidia nguvu za Kiuchumi
Visiwani Zanzibar iwapo mipango ya uhakika itawekwa ukiwemo utaratibu
maalum wa kufuatilia makubaliano yanayofikiwa ya pande mbili husika.
Balozi Hija aliueleza Ujumbe huo wa Zanzibar kwamba Ofisi ya Ubalozi
Nchini India iko tayari kuratibu masuala yote yatayohusika na mikataba
au makubaliano baina na Zanzibar na Taasisi au Serikali ya Jimbo
lolote Nchini humokatika uanzishwaji wa ushirikiano wa kisekta.

Alifahamisha kwamba ipo miradi inayofikia hatua ya kutiwa saini katika
uanzishwaji wake lakini kinachokosekana kuibuka kwa miradi hiyo na
hatimae mengine kufifia ni ukosefu wa ufuatiliaji wa miradi hiyo jambo
ambalo huwavunja moyo wale wanao nia thabiti ya kusaidia.

Balozi Hija alielezea faraja yake kutokana na ujio wa Ujumbe huo wa
Zanzibar Nchini India na kusema kwamba huo ni mwanzo mzuri wa
kufungua njia itakayotoa mwanga kwa Zanzibar kujitanua zaidi kiuchumi
Kimataifa.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema ziara hiyo ina lengo la kutengeneza Diplomasia juu ya
ushirikiano kati ya Zanzibar na India hasa katika sekta za Afya,
Kilimo, Biashara na hata Utalii.

Balozi Seif alisema India imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika
Sekta ya Afya kiasi kwamba wagonjwa wengi wa Zanzibar wanaosumbuliwa
na maradhi tofauti kama Moyo, Figo pamoja na magonjwa mengine hupata
huduma za matibabu katika Hospitali za India.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/3/2017.
Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi,Mohamed Hija kati kati akielezea fursa mbali mbali zilizopo Nchini India ambazo Zanzibar inaweza kuzichangamkia kwenye kikao cha Ujumbe
wa Zanzibar uliowasili Nchini humo kwa ziara ya Wiki Moja.

Balozi Hija alikuwa akikiongoza Kikao cha matayarisho cha Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Eros – Nehru Palace iliyopo Mjini New Delhi India.

Wa kwanza Kulia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Asha Ali Abdulla. Wa kwanza Kushoto ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Waziri asiye ya Wizara Maalum Dr. Sira Ubwa Mamboya na Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments: