Thursday, March 30, 2017

WAZIRI MKUU AWASHAWISHI WAWEKEZAJI KUTOKA MAURITIUS KUWEKEZA NCHINI,Awataka waje kujenga viwanda vya sukari, nguo na samaki


SERIKALI imepanga kuondoka katika uchumi wa chini na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 ambapo katika kufikia azma hiyo imeweka juhudi kwenye uanzishwaji wa viwanda mbalimbali kuanzia vidogo hadi vikubwa.

Mpango wa kufikia uchumi wa kati unalenga kuiwezesha serikali kujitegemea na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuweza kufikia azma hiyo.

Dira ya Taifa ya Maendeleo, imeainisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenge uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa Serikali imeweka sera na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye viwanda.

Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikwenda nchini Mauritius kumwakilisha Rais Dk. John Magufuli kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP).

Baada ya kumaliza uzinduzi huo Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali nchini Mauritius na kuhamasisha wawekezaji waje nchini ili kuongeza uzalishaji utakaokuza uchumi na kuongeza pato la taifa.



KIWANDA CHA SUKARI CHA ALTEO


Akiwa kiwandani hapo Waziri Mkuu alipata maelezo ya uendeshaji wake kuanzia hatua ya utayarishaji wa mashamba ya miwa hadi uzalishaji wa sukari.

Waziri Mkuu alifurahishwa na teknolojia ya kisasa inayotumika kiwandani hapo hali iliyomfanya ashawishike kuwashawishi wawekezaji hao kuja nchini kupanua uwekezaji kwa kuongeza mashamba ya miwa na uzalishaji wa sukari.

Kiwanda cha sukari kinachomilikiwa na kampuni ya Alteo kina uwezo wa kukamua tani 400 za miwa kwa saa na kuzalisha tani 170,000 za sukari kwa mwaka.

Kampuni ya Alteo inamiliki kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kwa ubia na Serikali ya Tanzania na kinazalisha tani 110,000 kwa mwaka.

Aidha, Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho na kuwashawishi waongeze maeneo ya uwekezaji nchini.

“Tekonolojia wanayoitumia katika uendeshaji wa kiwanda chao ni nzuri hivyo tumewashawishi waje kuongeza maeneo ya uzalishaji wa sukari nchini ili tuweze kukidhi mahitaji,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Tanzania kuna viwanda vitano vya sukari ambavyo ni Mtibwa, Mahonda (Zanzibar), TPC, Kilombero na Kagera ambavyo uzalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya ndani ya nchi kwa mwaka ni tani 420,000.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed amesema Zanzibar kuna kiwanda kimoja cha sukari ambacho uzalishaji wake haukidhi mahitaji kutokana na uhaba wa malighafi.

Dk. Khalid amewakaribisha kampuni ya Alteo kwenda Zanzibar kushirikiana na Serikali katika uwekezaji hususani kwenye viwanda vya sukari.

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Patrick de Labauve amesema wamekubali kuongeza maeneo ya uwekezaji wa mashamba ya miwa nchini.

Pia ameomba Serikali iwapatie fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro kwani kuna vivutio vingi vya utalii ukiwemo mlima Kilimanjaro.

Akizungumzia kuhusu ajira amesema kiwanda cha TPC kimeajiri wafanyakazi 3,000 wakiwemo 1,900 wa kudumu wa ndani utakaotosheleza mahitaji na kupata ziada.

Kusimamia mfumo mzima wa usambazaji wa sukari nchini ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wafanyabishara wenye tabia ya kuhodhi soko la sukari kwa lengo la kusababisha upungufu usio halisi wa sukari (artificial shortage).

Kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wazalishaji wa sukari wa ndani ya nchi.



KIWANDA CHA SAMAKI

Waziri Mkuu pia alitembelea kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha viongozi wa kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya samaki.

Amesema Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo aina mbalimbali za samaki.

Waziri Mkuu amesema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes kilichoko jijini Port Louis nchini Mauritius.

“Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema.

Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji waliotayari kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.

Dk. Khalid alisema lengo la uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Patrick Hill alisema wamefurahia mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali.

Alisema kampuni yao inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa wakiwa ni bara la Ulaya.



KIWANDA CHA NGUO

Akiwa kwenye kiwanda cha nguo cha Compagnie Mauricienne De Textile Ltee kinachotengeneza nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa nchini Mauritius chenye uwezo wa kutengeneza tani milioni 40 hadi 50 kwa mwaka.

Waziri Mkuu aliwakaribisha wawekezaji hao kuja nchini kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo kwa kuwa kuna malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji huo.

“Tumefarijika na uwekezaji wenu na tumejionea namna ambavyo mnavyoendesha kiwanda chenu kuanzia utengenezaji wa nyuzi hadi nguo, hivyo tunahitaji viwanda kama hivi nchini Tanzania kwa sababu sisi tunazalisha pamba nyingi na yenye ubora unaokubalika kimataifa,” alisema.

Waziri Mkuu alisema madhumuni ya kuwakaribisha wawekezaji hao kuja Tanzania na kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi yanalenga kuboresha kilimo cha pamba na kuwawezesha wakulima kupata tija.

“Tunalima pamba nzuri na hawa hawalimi wananunua kutoka nje ya nchi yao, hivyo wakija kuwekeza Tanzania itawarahisishia kupata malighafi ya uhakika na kwa urahisi ” alisema.

Alisema viwanda hivyo vitasaidia maendeleo ya kilimo cha pamba kwa sababu vitatoa ajira kwa wananchi wengi hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini wa kipato.

Mbali na kuwakaribisha wawekezaji hao, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuhakikisha wanajenga viwanda vya nyuzi kwenye mikoa yote inayozalisha pamba ili waweze kuiongezea thamani kabla ya kuiuza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho David Too Sai Voon alisema wamefurahishwa na mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya nyuzi na nguo.

David alisema kiwanda chao kilianzishwa mwaka 1986 na kwa sasa kimeajiri wafanyakazi 18,000 ambapo mauzo yao kwa ni dola milioni 200. “Nguo tunazotengeza ni za kiwango cha kimataifa na tunauza katika maduka makubwa barani Ulaya,”


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
SLP 980, DODOMA
ALHAMISI, MACHI 31, 2017.

No comments: