Thursday, March 9, 2017

Serikali yatoa rai kwa watanzania kununua hisa za Vodacom

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Ashatu Kijaji,  ameipongeza kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC kuwa ya kwanza kutekeleza sheria ya EPOCA na sheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa  kuuza hisa zake kwa Umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na alitoa rai kwa watanzania,makampuni ya kitanzania na taasisi za serikali kujitokeza kununua hisa hizo baada ya kusoma waraka  wa matarajio wenye mwongozo wa ununuaji wa hisa za kampuni hiyo.

Akiongea wakati wa Uzinduzi wa  uuzaji wa hisa za kampuni hiyo uliofanyika jijini Dar e salaam, Dkt.Kijaji alisema kuwa uwekezaji huu  utakuza shughuli za soko kwa asilimia kubwa “Hivi sasa wawekezaji katika hisa kwenye masoko ya mitaji hapa nchini ni takribani laki tano,hivyo iwapo wateja wote wa Vodacom milioni 12.4 watashiriki katika ununuzi wa hisa utaongeza uwekezaji wa hisa kupitia masoko ya mitaji  katika soko la hisa kwa asilimia 2,380%.

Alisema haya  yatakuwa ni mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji na fedha si hapa nchini tu bali hata katika ukanda wa Afrika Mashariki kwani hivi sasa Kenya ina wawekezaji wapatao 1,700,000,Uganda 40,000 na Rwanda 14,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Ian Ferrao amesema, “Tunayo furaha kuifikia siku  ya leo ambapo tumefungua milango kwa wananchi wa Tanzania na  tunawakaribisha wanaotaka kuwekeza katika safari hii ambayo tumeianza.Tukio hili ni la kihistoria katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania, Vodacom Tanzania imekuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano hapa nchini kuandika historia ya kuuza hisa zake kwa umma kupitia Soko la benki ya NBC yenye matawi nchi nzima na mawakala kwa kuuza hisa kuwashirikisha watanzania wote katika safari ya mafanikio ya kampuni yetu”.

Ferrao alisema kuwa kuanzia  leo,asilimia 25% za kampuni ya Vodacom Tanzania PLC zitauzwa kwa watanzania kutokana na kibali kutoka serikalini kupitia Mamlaka ya Dhamana Masoko na mitaji (CMSA)-“Kutokana na matakwa ya sheria hadi kufikia hatua hii tumepata ushirikiano mkubwa kutoka taasisi za serikali za CMSA ,DSE na wadau wengine,nashukuru kwa ushirikiano huu ambao umefanikisha mchakato mzima na leo wateja wetu nchini kote na taasisi mbalimbali za kitanzania zinazo fursa ya wabia  wetu kupitia ununuaji huu wa hisa”Aliongeza.

Kuhusiana na mchakato mzima wa ununuaji wa hisa alisema “Kutokana na kuzinduliwa mchakato wa uuzaji hisa kuanzia leo,wanaohitaji kununua hisa watazipata kwa kutembelea matawi yote ya Benki ya NBC  na mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) waliopo nchi nzima “.Alitoa msisitizo kuwa kila hisa itauzwa kwa shilingi 850/-na asilimia 25% ya hisa zinazotarajiwa kuuzwa zina thamani ya shilingi Bilioni  476.

Ferrao alimalizia kwa kusema “Vodacom Tanzania PLC inayo dhamira ya kweli ya kuendelea kuwekeza nchini na kukuza sekta ya mawasiliano na kufanikisha malengo yake makuu ambayo ni kuwapeleka watanzania katika ulimwengu wa kidigitali,kuwaunganisha watanzania katika mtandao wake na kubadilisha maisha ya wananchi kuwa murua kupitia ubunifu mkubwa wa kiteknolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Ian Ferrao(kushoto)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari na wageni waalikwa(hawapo pichani)wakati wa Uzinduzi wa Uuzaji wa hisa za kampuni hiyo kwa Umma leo jijini Dar es Salaam,Waliokaa kutoka kushoto ni Mkuu wa kitengo cha huduma za kibenki kwa makampuni wa NBC,Theobald Sabi, Mkuu wa kitengo cha huduma za Uwekezaji wa hisa za makampuni wa Orbit Securities,Godfrey Gabriel na Mkurugenzi wa fedha wa Vodacom Tanzania PLC, Jacques Marais.

Naibu Waziri wa fedha na Mipango,Dkt.Ashuta Kijaji(watatu kushoto) Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Ian Ferrao(kushoto kwake)Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimazi wa Mawasiliano(TCRA) Eng.James Kilaba(kushoto)Mwenyekiti wa bodi ya Vodacom Tanzania PLC,Vivek Mathur(wanne kushoto)na Mkurugerugenzi wa kitengo cha biashara za Vodacom Tanzania PLC,Gregory Verbond,wakiponyeza kitufe kuashiria Uzinduzi wa Uuzaji wa hisa za Vodacom Tanzania PLC kwa Umma leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa fedha na Mipango,Dkt.Ashuta Kijaji(katikati)akiagana na Mwenyekiti wa bodi ya Vodacom Tanzania PLC,Vivek Mathur(kulia)baada ya kuzindua Uuzaji wa hisa za Vodacom Tanzania PLC kwa Umma leo jijini Dar es Salaam,kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ian Ferrao.
Naibu Waziri wa fedha na Mipango,Dkt.Ashuta Kijaji(kushoto)akimsikiliza jambo Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Ian Ferrao,baada ya kuzindua rasmi Uuzaji wa hisa za Vodacom Tanzania PLC kwa Umma leo jijini Dar es Salaam.
Kutoka kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Ian Ferrao,Mkuu wa kitengo cha huduma za kibenki kwa makampuni wa NBC,Theobald Sabi,Mkurugenzi wa fedha wa Vodacom Tanzania PLC, Jacques Marais,Wakimsiki Mkuu wa kitengo cha huduma za Uwekezaji wa hisa za makampuni wa Orbit Securities,Godfrey Gabriel(katikati)alipokuwa akijibu swali kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)wakati wa Uzinduzi wa Uuzaji wa hisa za kampuni hiyo kwa Umma leo jijini Dar es Salaam.

1 comment:

Unknown said...

Hisa moja ni shilingi ngapi?.. Nataka kuwekeza Mimi chap