Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiruka mtaro
wa maji uliopo pembezoni mwa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1
inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Muonekano
wa sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango
cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera. Barabara hiyo inajengwa na
mkadarasi kutoka Kampuni ya CHICO na imegharimu kiasi cha Shilingi
Bilioni 64.96.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Mhandisi Jumanne Werema (wa kwanza kulia), kuhusu
kukamilisha ujenzi kwa wakati wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la
Mafumbo, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Mhandisi
Jumanne Werema kutoka Kampuni ya ujenzi wa CMG akimpa taarifa ya mradi
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu
hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la
Mafumbo, wakati alipokagua, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati),
akiongozana na Mhandisi Salum Chanzi (kushoto), kutoka Wakala wa Majengo
nchini (TBA), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro
(kulia), kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana
ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban
miezi sita iliyopita.
Moja
ya Jengo la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo linalojengwa na
Wakala wa Majengo Nchini (TBA), baada ya Shule hiyo kuathiriwa na
tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita, mkoani Kagera.
Mhandisi
Mshauri wa Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa kutoka Wakala
wa Barabara Nchini (TECU), Eng. Mushubira Kamuhabwa (kulia), akitoa
taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa (kushoto), kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene KM
59.1 kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
………………..
Serikali
imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na
kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya
hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya
kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani
ya kulipwa fidia na Serikali.
“Najua
bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa
nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote
anayevunja sheria”, amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza
Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara
hiyo kwa kuzingatia viwango na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo
hicho ili kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha,
amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda
na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama
ilivyokusudiwa.
Kwa
upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa,
amesema kuwa kazi inaendelea vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika
asilimia 98 ambapo kazi iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.
Eng.
Kamuhabwa ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha
usafirishaji wa mizigo na abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo
kati ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Mradi
wa ujenzi wa barabara ya Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya
CHICO kutoka nchini China na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 64.96.
Katika
hatua nyengine Waziri Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya
ujenzi wa shule ya Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera
iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Akiwa
katika shule hiyo Profesa Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi
anayejenga shule hiyo na kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo
kwa ubora wa hali ya juu ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine
ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo
kwa ubora wa hali ya juu.
Ni
takribani miezi sita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera
na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja,
hospitali, shule pamoja na makazi ya watu.
Kutokana na uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo.
No comments:
Post a Comment