Na: Lilian Lundo - MAELEZO
Tume iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza kifo cha Faru John imethibitisha kuwa Faru huyo alikufa katika eneo la Sasakwa Grumeti kutokana na kukosa matunzo, uangalizi wa karibu na matibabu alipoumwa.
Hayo yamesemwa leo Jijini, Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele alipokuwa akikabidhi ripoti ya uchunguzi wa Kifo cha Faru huyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
“Sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba ni mifupa ambayo ilichukuliwa katika mzoga wa Faru John uliokutwa eneo la Sasakwa Grumeti, Pembe zilizochukuliwa hifadhi ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), damu kutoka maabara ya NCAA na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), ngozi kutoka kwenye mzoga na kinyesi kilichokaushwa kutoka SUA,” alifafanua Prof. Manyele.
Aliendelea kwa kusema kuwa matokeo ya uchunguzi wa awali yameonyesha damu, pembe, mifupa na ngozi ni vya Faru John ambapo mpangilio wa vinasaba umeonyesho kuwa Faru huyo ni mweusi (Black Rhinoceros) mwenye jinsia ya kiume.
Aidha vielelezo hivyo vilitumwa Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini ambapo timu ya wataalam kutoka Tanzania chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali walishiriki katika uchunguzi wa awali wa vinasaba na kujadili matokeo kabla ya kuyatuma kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo Matokeo yameonyesha sampuli na vielelezo vyote ni vya mnyama pori Faru John.
Vile vile amesema, uchunguzi umeonyesha kuwa sababu za kifo cha Faru huyo ni kukosa matunzo, uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria pamoja na mapungufu ya kiuongozi kwa Wizara, Hifadhi na Taasisi zake.
Baadhi ya mapungufu yaliyobainishwa katika uchunguzi huo ni pamoja na kutokuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti.
Prof. Manyele amesema kuwa hakukuwa na mkataba rasmi kati ya Serikali na mwekezaji unaoonyesha mnyama ametoka Serikalini kwenda kwa Mwekezaji.
Tume hiyo imeishauri Serikali kuchunguza viwanja vya ndege ndani ya hifadhi vinavyomilikiwa na wawekezaji kutokana na kuwepo na uwezekano wa viwanja hivyo kuwa njia ya majangili au matajiri kufanikiisha shughuli za ujangiri nchini.
Aidha kutokana na mapungufu ya kiutendaji yaliyofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini (kutokutoa kibali rasmi) na mapungufu ya kiuongozi yaliyofanywa na Mhifadhi wa NCAA kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali, Tume inashauri hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza timu hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya. Ameahidi kufanyia kazi maoni ya tume hiyo na kutolea maelezo ya hatua zitakazochukuliwa na Serikali muda mfupi ujayo.
Tume ya uchunguzi ya kifo cha Faru John iliundwa baada ya Waziri Mkuu kufanya ziara ya kikazi Ngorongoro Disemba 6, 2016, ambapo alibaini kuhamishwa kinyemela kwa faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumeti.
Waziri Mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa Faru huyo na kuamua kuunda tume hiyo ili kubaini ukweli wa Faru huyo kama alikufa au alitoroshwa.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kulia akipokea taarifa ya Tume aliyounda kuchunguza kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele jijini Dar es Salaam leo
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kulia akionyesha taarifa ya Tume aliyounda kuchunguza kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele jijini Dar es Salaam leo
No comments:
Post a Comment