Wednesday, March 29, 2017

REA YAMWONDOA MKANDARASI MZEMBE




Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye kipaza sauti) akiwatambulisha wafanyakazi wa Kampuni ya Nakuroi Investment Co. Ltd (waliochuchumaa), ambao watatekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Singida.
Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mkwese, wilayani Manyoni.
Moja ya vikundi vya ngoma kutoka Manyoni, kikitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mkwese, wilayani Manyoni.


Na Veronica Simba – Dodoma

Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umesitisha mkataba wa Mkandarasi Spencorn Services, aliyekuwa akitekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya pili kwa Mkoa wa Singida.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga aliyasema hayo hivi karibuni katika hafla ya uzinduzi wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida, uliofanyika kijijini Mkwese, wilayani Manyoni.

Mhandisi Nyamo-Hanga alimweleza Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Mradi huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, ufanisi wa kazi wa Mkandarasi husika haukuwa mzuri hivyo kusababisha baadhi ya vijiji ambavyo vilipangwa kupelekewa umeme katika REA II, kutofikiwa na huduma hiyo.

“Tumechukua hatua za kinidhamu. Tumemsimamisha kazi na tutaleta wakandarasi wapya ambao wataendelea na kazi ya kusambaza umeme pale alipoishia.”

Aidha, Mkurugenzi Nyamo-Hanga alitoa shukrani kwa Serikali kwa ushirikiano na msaada ambao imekuwa ikitoa, ulioiwezesha REA kuendelea na zoezi la kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini kwa mafanikio makubwa.

Alisema kuwa, gharama ya utekelezaji wa REA III Mkoa wa Singida ni shilingi bilioni 47.36 ambapo jumla ya vijiji vitakavyonufaika ni 267. Aliongeza kuwa, Mkandarasi atakayetekeleza Mradi huo ni Nakuroi Investment Co. Ltd.

“Tutaanza na kuunganisha umeme katika vijiji 185 na baadaye tutamalizia vijiji 82 vitakavyokuwa vimebaki, na kuwezesha vijiji vyote vya Mkoa wa Iringa kuwa na umeme kwa asilimia 100.”

Idadi ya vijiji vilivyo na umeme hadi sasa kwa Mkoa wa Singida ni 196, sawa na asilimia 42.

Mhandisi Nyamo-Hanga, amewataka wananchi watakaounganishiwa umeme katika Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Tatu, kama ilivyokuwa kwa Mradi wa Awamu ya Pili; kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili wakati mkandarasi atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.

Vilevile, ameomba Serikali za Kata na Vijiji kubainisha maeneo maalum ya viwanda ambayo katika mradi huu, yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa ili kuwezesha wajasiriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama nafuu.

Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaendelea katika Mikoa mbalimbali nchini. Mpaka sasa, uzinduzi umekwishafanyika katika Mikoa ya Tanga, Pwani, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songwe, Mara na Singida. Kwa Mkoa wa Shinyanga, uzinduzi utafanyika tarehe 1 Aprili, mwaka huu.

No comments: