Friday, March 24, 2017

Prof Mbarawa alivyopamba sherehe za miaka 100 za benki Standard Chartered

 WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amezialika benki nchini kushiriki katika kutoa mikopo ya riba nafuu katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwamo katika sekta za miundombinu.

Profesa Mbarawa alisema hayo juzi usiku wakati alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 100 ya shughuli za Benki ya Standard Chartered nchini, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa benki hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini.

Waziri huyo alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, pamoja na mambo mengine, imechukua hatua kadhaa katika kuhakikisha Taifa linapiga hatua kiuchumi ikiwamo kuimarisha miundombinu, kupambana na rushwa na kuongeza ufanisi katika serikali.

Alisema Tanzania ni nchi ya 11 ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kwa mujibu kwa takwimu za 2015 (unakua kwa asilimia saba) na kwa Afrika, ni ya sita kwa nchi ambazo uchumi wake wa viwanda unakua kwa kasi.

“Nafahamu kwamba Benki ya Standard Chartered ina uzoefu mkubwa wa kuunga mkono miradi ya miundombinu katika Afrika na sehemu nyingine duniani, kwa hiyo wakati mnapoadhimisha miaka 100 ya shughuli zenu nchini Tanzania, itakuwa jambo jema kama mtafanya tathimini ya fursa za kuwekeza katika miradi ya miundombinu ya usafiri na sekta nyingine ambazo ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano,” alieleza Profesa Mbarawa.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, ujenzi wa barabara tano za juu katika makutano ya baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam, ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari na vyombo vya usafiri wa majini.

“Kwa hiyo, ninaziomba benki nchini kuja kuzungumza na serikali na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kusaidia miradi ya kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Tano. Tunaikaribisha Standard Chartered na benki nyingine kutumia fursa hii ya serikali kujitokeza kufadhili miradi hiyo, lakini tunasisitiza kuwa lazima waje na mikopo yenye riba nafuu ili Watanzania wasibebeshwe mzigo mkubwa wa kulipa fedha hizo,” aliongeza Profesa Mbarawa.

Aliisifu benki hiyo kwa kazi nzuri inayofanya nchini, na kufikisha miaka 100 ni mafanikio makubwa ya kupongezwa na pia kuonesha inavyoijali Afrika na hasa Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani aliahidi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wao.

Alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kukuza uchumi wa nchi kwa kutoa huduma bora na stahiki kwa wananchi na kuchangia kutimiza dhana ya Tanzania ya Viwanda kufikia mwaka 2015.

Akizungumzia uwepo wa ujumbe mzito wa viongozi wa benki hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani, Rughani, alisema, “Hii ni kwa mara ya kwanza kwa benki hiyo hapa nchini kuwa na ujumbe mzito kama huu, hii inaonesha ni kwa kiasi gani wana imani na utendaji wa kazi wa benki hii kwa hapa nchini.. Ikiwa imeanza kazi hapa nchini mwaka 1917, benki hiyo imekuwa ikiwahudumia Watanzania wengi hapa.

 WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 100 ya shughuli za Benki ya Standard Chartered nchini, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa benki hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini.
  WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (pichani kushoto) akishiriki hafla ya  maadhimisho ya miaka 100 ya shughuli za Benki ya Standard Chartered nchini, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa benki hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini.
 Baadhi ya viongozi wa juu wa benki Standard Chartered nchini kutoka sehemu mbalimbali Duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini wakifuatilia yaliyokijiri ukumbini humo.
  Baadhi ya viongozi wa juu wa benki Standard Chartered nchini kutoka sehemu mbalimbali Duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini wakifuatilia yaliyokijiri ukumbini humo.
 Wageni waalikwa mbalimbali
Baadhi ya viongozi wa juu wa benki Standard Chartered nchini kutoka sehemu mbalimbali Duniani pamoja na wateja wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini wakifuatilia yaliyokijiri ukumbini humo.

No comments: