Wednesday, March 29, 2017

MTANZANIA ALIYEWEKA REKODI YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO KWA MUDA MFUPI AMUANGUKIA WAZIRI MWAKYEMBE


Gaudence Lekule akiwa katika kilele cha Uhuru ,Mlima Kilimanjaro baada ya kukimbia kwa muda wa wa saa 8:36 mpya akiwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza kutumia muda huo kupanda kilele cha mlima Kilimanjaro na kushuka.

Gaudence Lekule akipanda mlima Kilimanjaro huku akikimbia wakati akiweka rekodi baada ya kutumia muda wa saa 8:36 mapema mwaka huu.
Lekule akifurahia mara baada ya kufanikiwa kuweka ekodi ya kutumia muda wa saa 8:36 kupanda Mlima Kilimajaro na kushuka.


Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

MTANZANIA ,Gaudence Lekule (31) anayeshiriki michezo ya kupanda milima kwa kasi (Mountain Run) amemuomba Waziri mpya wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo ,Dkt Harison Mwakyembe kutupia jicho michezo mingine kwani ina nafasi kubwa ya kutangaza na kuletea sifa taifa.

Lekule anayeshikilia rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza Duniani kupanda kwa muda mfupi katika Mlima Kilimanjaro akitumia muda wa jumla wa saa 8:36 alitoa wito pia kwa kampuni,taasisi binafsi na za serikali kujitokeza kudhamini wanamichezo kutokana na eneo hilo upo uwezekano wa kujitangaza zaidi kidunia.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum,Gaudence alisema kwa sasa yupo katika maandalizi ya kuweka rekodi mpya katika milima mirefu na maarufu Duniani kwa kufanya mazoezi ya awali hapa nchini na baadae nje ya nchi.

“ Nashukuru kuitangaza Tanzania kidunia na tayari nimepata mialiko mingi ya kwenda nje kushiriki mashindano ya Mountain Run ,Lengo langu ni kuweka rekodi katika milima mirefu duniani hivyo bado naendelea na mazoezi na nitaendelea kufanya mazoezi hapa kwetu na badaae nje ya Tanzania”alisema Gaudence .

Alisema hadi sasa rekodi ya Dunia inashikiliwa na raia wa nchi ya Ecuador, Karl Egloff aliyetumia muda wa saa 6:53 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro ,rekodi aliyoweka mwaka 2014 akivunja rekodi ya Kilians Jornet raia wa Hispania aliyetumia muda wa saa 7:20 kupanda na kushuka mlima Kilimanjaro mwaka 2010.

Lekule alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni mabadiliko hali ya hewa inayochangia kushindwa kufanya mazoezi na upatikanaji wa mahitaji kama chakula pamoja na mavazi kwa ajili ya mchezo huo unafanyika kuanzia urefu wa mita 3500 hadi 5800.

Akizungumzia kilichomsukuma kushiriki mcezo mchezo huo,Lekule ,mkazi wa kiraracha Marangu wilaya ya Moshi alisema raia wa kigeni wamekuwa wakishiriki katika michezo ya aina hiyo kwa ajili ya kuweka rekodi hivyo akaona ni wakati wa waafrika pia kushiriki katika uwekaji wa rekodi Duniani.

Alisema raia wa Ecuador ,anayeshikilia rekodi ya dunia aliposikia ameweka rekodi akiwa ni mwafrika na Mtanzania wa Kwanza alituma salamu za pongezi huku akimtaka kwenda kwenye milima iliyopo nchi za nje kutafuta rekodi nyinine.

“ Egloff alifurahi sana na kunipa moyo na kunitaka nikatafute rekodi nje ya Afrika kwa sababu nina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri Ulaya na kuipa sifa Tanzania,ni ngumu sana mtu kukimbia kwenye urefu kama uliopo Mlima Kilimanjaro na katika maisha inahitaji moyo sana.”alisema Lekule.


Rekodi za kidunia.

Mara ya kwanza rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kasi kwa Afrika ilikua inashikiliwa na Saimon Mtui akitumia muda wa saa 9 : 20 mwaka 2006, baadae raia wa Hspania Kilians Jornet alitumia muda wa saa 7:20 mwaka 2010.

Mwaka 2014 ndipo Karl Egloff raia wa Ecuador anayeshikilia rekodi ya Dunia hadi sasa alitumia muda wa saa 6 :53 mwaka 2014 na sasa Mtanzania Gaudence Lekule ameweka rekodi ya kuwa Muafrika na Mtanzania wa Kwanza akitumia muda wa saa 8:36 .

No comments: