Wednesday, March 8, 2017

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI TANZANIA AFANYA ZIARA MKOANI KAGERA KUKAGUA UJENZI WA KITUO CHA AFYA KABYAILE MISSENYI

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amefanya ziara ya kikazi Mkoani Kagera kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kabyaile Wilayani Missenyi kinachojengwa upya na Jeshi la Wananchi Tanzania mara baada ya kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mwezi Septemba mwaka jana.

Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo alifanya ziara hiyo Machi 2, 2017 na lengo kuu ilikuwa ni kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho mara baada muda alioutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuisha mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu 2017.

Rais Magufuli alipofanya ziara Mkoani Kagera Januari 1, 2017 alitembelea eneo la Kabyaile Wilayani Missenyi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na kuagiza kuwa ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo Mwisho mwa mwezi Februari 2017.

Mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo akiongea na viongozi wa mkoa na wananchi waliofika kumuona kituoni hapo alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo, pia alishukuru upanuzi wa majengo kuwa ni manufaa kwa wananchi wa Kabyaile na Wilaya ya Missenyi kwa ujumla.

Pia aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania kinachojenga kituo hicho kuwa kikosi hicho kinafanya kazi katika hali ya utulivu na amani na wananchi wenyeji, aidha aliwaomba wananchi kuwaona wananjeshi kama raia wengine na kuendelea kuwapa ushirikiano kwani wanatokana na Watanzania wenyewe.

Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo baada ya kukagua ujenzi na kupata maelezo ya kina alisema kuwa muda alioutoa Rais Magufuli wa hadi mwishoni mwa Mwezi Februari 2017 ujenzi haukuweza kukamilika kwasababu kuna kazi zingine za ziada ambazo zilijitokeza na kushindwa kukamilisha kituo hicho kwa muda uliotolewa.

?Kwa kazi alizoelekeza Rais Magufuli tayari zipo katika hatua za mwisho kabisa za umaliziaji, pia na kazi zilizoongezeka zipo katika hatua nzuri ya ujenzi na kufikia mwishoni mwa mwezi Machi 2017 kazi zote zitakuwa zimekamilika zote? Aliwaeleza wananchi Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Jenerali Mabeyo alitembelea pia ujenzi wa Shule ya Sekondari Omumwani Katika Manispaa ya Bukoba kunakojengwa vyumba viwili vya mabweni na Kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania, aidha alimalizia ziara yake katika Shule ya Sekondari Ihungo na kukagua ujenzi mpya wa shule hiyo iliyoharibiwa na tetemeko pia mwezi Septemba Mwaka jana 2016.

No comments: